Kukaribia kushindwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24673-kukaribia_kushindwa_genge_la_kigaidi_la_daesh_(isis)_nchini_iraq
Yan Kubish, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq amesema kuwa, kushindwa kikamilifu kundi la kigaii la Daesh kumekaribia na kwamba msaada wa jamii ya kimataifa kwa Wairaki, baada ya kushindwa kundi hilo ni suala muhimu sana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2017 03:19 UTC
  • Kukaribia kushindwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Iraq

Yan Kubish, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq amesema kuwa, kushindwa kikamilifu kundi la kigaii la Daesh kumekaribia na kwamba msaada wa jamii ya kimataifa kwa Wairaki, baada ya kushindwa kundi hilo ni suala muhimu sana.

Operesheni za kuusafisha mji wa Mosul kutokana na uepo wa wanachama wa kundi la Daesh (ISIS) zilianza tarehe 17 Oktoba mwaka jana. Huku ikiwa imepita miezi mitatu tangu kuanza operesheni hizo, tarehe 24 mwezi Januari mwaka huu, Haider al-Abadi Waziri Mkuu wa Iraq alitangaza kusafishwa kikamilifu eneo la kushoto la ukingo wa mji wa Mosul kutokana na uepo wa wanachama wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu, sambamba na kutaka kuanzishwa pia operesheni kali katika upande wa kulia wa ukingo wa mji huo. Kabla ya kuanza operesheni za kuukomboa mji huo, kulishadidi hujuma za vyombo vya habari vya upinzani wa serikali ya Iraq dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Shabi na kutokana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya vikosi vinavyoshiriki operesheni hizo, harakati hiyo ikazuiwa kuingia mjini Mosul.

Wanachama wa genge la Daesh wakikimbia ovyo baada ya kuzidiwa na jeshi la Iraq

Kadhalika vyombo hivyo vya habari vililituhumu jeshi la Iraq kwa madai ya kuhusika na ukandamizaji dhidi ya raia, tuhuma ambazo hata hivyo zimepingwa na serikali ya Baghdad. Kufuatia hali hiyo, Yan Kubish, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq amenukuliwa akithibitisha kufungamana jeshi la Iraq na misingi ya kisheria katika utekelezaji wake wa operesheni za kuukomboa mji wa Mosul. Suala lingine ambalo limekuwa likizungumziwa kuhusiana na operesheni za kuukomboa mji huo na ambalo limesisitizwa na mwakilishi huyo wa UN, ni suala zima la usimamizi wa mji wa Mosul baada ya kuondoshwa wanachama wa kundi hilo. Kadhia hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kiasi cha kuibua tofauti za kimtazamo hususan kwa wanasiasa wa upinzani wa ndani na nje ya nchi hiyo, kwa lengo la kutaka kudhoofisha nafasi ya serikali ya Baghdad katika kipindi hiki muhimu.

Jeshi la Iraq likifuatilia kwa karibu nyendo za wanachama wa Daesh

Ni vyema ikafahamika kuwa, Mosul na mkoa wa Nainawa (Nineveh) kwa ujumla, umekuwa na umuhimu mkubwa nchini Iraq, huku usimamizi wake ukiwa mikononi mwa serikali kuu ya nchi hiyo. Hata hivyo tofauti za kimtazamo zinazotolewa na viongozi wa eneo la Kurdistan kuhusiana na suala hilo, si tu kwamba zimesababisha kucheleweshwa operesheni za kuukomboa mji huo kutokana na uepo wa wanachama wa genge hilo la kigaidi bali  pia zimawaletea wasi wasi mkubwa wakazi wa mji huo. Ni kutokana na suala hilo, ndipo Yan Kubish, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq akanukuliwa akisema kuwa, kukosekana msaada na usimamizi wa serikali ya Baghdad baada ya kukombolewa mji wa Mosul, kuna maana ya kukaririwa makosa yale yale yaliyowahi kufanywa huko nyuma, suala ambalo litakuwa na matokeo mabaya kwa usalama na uthabiti wa ndani na nje ya mipaka ya Iraq.

Wanajeshi wa Iraq wakiangalia vitu vilivyoachwa na magaidi wa Daesh baada ya kukimbia

Suala ambalo linaonekana katika matamshi ya mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq si tu kwamba linahusiana na kadhia ya 'Mosul baada ya Daesh', bali linahusiana na ulazima wa kuungwa mkono serikali ya Baghdad baada ya kuondoshwa kundi hilo mjini humo. Matamshi hayo kwa upande mmoja yana maana ya kukiri Yan Kubish, kukaribia kushindwa kikamilifu kundi hilo la kigaidi, na kwa upande wa pili udharura wa kutojitenga maeneo ya Mosul baada ya ukombozi wake. Katika hali ambayo suala hilo linaonekana kuziathiri pande mbalimbali za ndani na nje ya Iraq, msimamo wa Kubish unaweza kuwa hatua muhimu kwa ajili ya kuimarisha usalama, amani na mshikamano wa kijamii na kisiasa nchini Iraq baada ya kuondoshwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika ardhi ya nchi hiyo, kundi ambalo linaungwa mkono na Marekani, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Saudia na Qatar.