HRW yatiwa wasiwasi na kuongezeka mateso Saudi Arabia
Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema linatiwa wasiwasi na kuongezeka pakubwa mateso nchini Saudia.
Sarah Whitson Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kuwa Saudi Arabia inafanya juhudi za kumnyamazisha au kumtia nguvuni mtu yoyote ambaye hafuati siasa zake. Bi Whitson ameeleza pia kuwa iwapo mtu atatokea kufanya mazungumzo na vyombo vya habari au taasisi zisizo za kiserikali za kigeni huko Saudia ataishia kukamatwa na kuteswa na kwamba raia wanaotiwa mbaroni hutuhumiwa kwa kosa la kutomtii Mfalme, kuvunja baiya yao kwa utawala ulioko madarakani na kushiriki maandamano yaliyopigwa marufuku.
Ripoti mpya ya Human Rights Watch imemuashiria pia Nadhir al Majid mwandishi aliye na umri wa miaka 39 raia wa Saudia ambaye tarehe 18 Januari alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela na kupigwa marufuku kwa miaka 7 kutoka nje ya nchi kwa kosa la kushiriki katika maandamano ya wananchi mwaka 2011 dhidi ya utawala wa Aal Saud. Mwandishi huyo anashikiliwa katika jela moja karibu na mji wa Riyadh huku akizuiwa kuwasiliana hata na familia yake.