UN: Israel imevuka mstari mwekundu kwa kuidhinisha ujenzi haramu
(last modified Wed, 08 Feb 2017 03:34:13 GMT )
Feb 08, 2017 03:34 UTC
  • UN: Israel imevuka mstari mwekundu kwa kuidhinisha ujenzi haramu

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa Israel imekanyaga mstari mwekundu kwa kupasisha sheria ya kuhalalisha ujenzi mpya wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa Kizayuni.

Nickolay Mladenov, Mshirikishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kile kinachoitwa kuwa ni mchakato wa amani Mashariki ya Kati jana Jumanne aliutaja uamuzi huo wa Bunge la Israel (Knesset) kuunga mkono ujenzi haramu katika ardhi za Palestina kuwa ni 'hatari sana na wenye taathira hasi'.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa UN amesisitiza kuwa, sheria hiyo ambayo itafungua mlango kughusubiwa ardhi yote ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan inavuruga mchakato wa amani na ametoa wito wa kulaaniwa na kukosolewa kimataifa sheria hiyo.

Upanuzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi, Palestina

Mshirikishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani Mashariki ya Kati amebainisha kuwa, sheria hiyo mpya ya Israel imeongeza uwezekano wa utawala huo bandia kufunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jina (ICC).

Kadhalika jana Jumanne Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilikosoa vikali sheria hiyo tata ya Israel ikisisitiza kuwa, sheria hiyo ni pazia tu la kuhalalisha wizi wa ardhi za Wapalestina.

Hivi karibuni, Michael Lynk, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu alilitaka Baraza la Usalama na Baraza Kuu la umoja huo kuchukua hatua za lazima za kidiplomasia na kisiasa kwa ajili ya kuulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel uheshimu pamoja na kutekeleza azimio nambari 2334.

Baraza la Usalama la UN

Ikumbukwe kuwa, Disemba 6 mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 ambalo lililaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo ya Wapalestina.

Tags