Hujuma ya anga ya Israel huko Gaza yaua, kujeruhi Wapalestina 7
Kwa akali Wapalestina wawili wameuawa shahidi huku wengine zaidi ya watano wakijeruhiwa baada ya ndege ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutekeleza hujuma ya anga katika mji wa Rafah, Ukanda wa Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Duru za habari huko Palestina zimearifu kuwa, shambulizi hilo la mapema leo la ndege ya utawala haramu wa Israel lililenga barabara ya chini ya ardhi ambayo imekuwa ikitumiwa na Wapalestina wa Gaza kuingiza chakula na bidhaa zingine za dharura katika ukanda huo.
Shirika la habari la al-Yawm limeripoti kuwa, hujuma hiyo ya kinyama katika mpaka wa Ukanda wa Gaza na Peninsula ya Sinai nchini Misri imeua shahidi kijana wa miaka 24 Hessam Hamid al-Soufi na mwingine wa miaka 38 Mohammad Anwar al-Aqra huku waliojeruhiwa wakipelekwa katika Hospitali ya Youssef al-Najjar, mjini Rafah.

Haya yanajiri siku tatu baada ya Wapalestina wengine kadhaa kujeruhiwa, kufuatia shambulizi la ndege za kijeshi za utawala katili wa Israel, lilolenga mashamba ya Wapalestina katika mji wa Khan Yunis, yapata kilomita 25 kusini mwa Gaza.
Itakumbukwa kuwa, uvamizi wa kijeshi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Gaza mwaka 2014, ulisababisha Wapalestina 2,200 wakiwemo watoto wadogo zaidi ya 500 kuuawa shahidi na askari katili wa Israel.
Ukanda wa Gaza umekuwa katika mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, tokea mwaka 2007.