Uingereza yaendelea kuiuzia silaha Saudia licha ya upinzani mkali wa kimataifa
Ripoti iliyofichuliwa nchini Uingereza imeonesha kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ameitaka serikali ya London kuendelea kuuzia silaha utawala wa Saudi Arabia unaoua watu wasio na hatia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo.
Ripoti hiyo inasema, mwezi mmoja tu baada ya ndege za kivita za Saudi Arabia kushambulia majlisi ya maombolezo iliyofanyika mjini Sanaa na kuua watu wasiopungua 140, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson alimshinikiza Waziri wa Masuala ya Biashara ya Kimataifa wa nchi hiyo, Liam Fox kuendelea kuiuzia silaha Saudi Arabia licha ya malalamiko na upinzani mkubwa wa wanasiasa na jumuiya za kutetea haki za binadamu.
Katika barua yake iliyofichuliwa jana na gazeti la The Guardia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alimtaka Liam Fox kutazama upya uamuzi wake wa kusitisha mkataba wa mauzo ya silaha kwa utawala wa Saudi Arabia.
Waziri wa Biashara ya Kimataifa wa Uingereza, Liam Fox alisimamisha mkataba wa mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia baada ya nchi hiyo ya kifalme kushambulia majlisi ya maombolezo mjini San'a na kuua raia wasiopungua 140.
Uingereza na Marekani zinakosolewa sana kutokana na kuendelea kuiuzia Saudi Arabia silaha za aina mbalimbali ambazo zinatumiwa kuua raia wasio na hatia nchini Yemen.