Hamas yateua kiongozi wake mpya Ukanda wa Ghaza
(last modified Tue, 14 Feb 2017 03:16:09 GMT )
Feb 14, 2017 03:16 UTC
  • Hamas yateua kiongozi wake mpya Ukanda wa Ghaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Palestina, Hamas, imemteua afisa wa ngazi za juu wa tawi lake la kijeshi kuwa kiongozi wa harakati hiyo Ukanda wa Ghaza.

Siku ya Jumatatu Hamas ilimteua Yahya Sinwar, kamanda wa ngazi za juu wa Brigedi la Ezzedine Qassam kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo katika Ukanda wa Ghaza.

Sinawar atachukua nafasi ya Ismail Haniya, ambaye alikuwa waziri mkuu wa harakati ya Hamas wakati chama hicho kiilipochaguliwa kidemokrasia kuongoza eneo hilo mwaka 2007. Weledi wa mambo wanasema, kuna uwezekano mkubwa Haniya akachukua nafasi ya Khaled Mashaal, mkuu wa idara ya kisiasa ya Hamas na ambaye anaishi uhamishoni katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

Yahya Sinwar, mkuu mpya wa harakati ya HAMAS Ukandawa Ghaza

 

Halikadhalika Khalil al-Haya amechaguliwa kuwa naibu wa Sinwar katika mabadiliko hayo mapya ya uongozi wa Hamas.

Sinwar ambaye ana umri wa miaka 55 ni mwanzilishi wa Brigedi ya Ezzedine Qassam, tawi la kijeshi la Hamas. Sinwar alitekwa nyara na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1988 na kuachiliwa huru mwezi Oktoba mwaka 2011 katika mapatano ya mabadilishano ya wafunwa ambapo Wapalestina 1,000 waliachiliwa huru mkabala wa mwanajeshi mmoja wa Israeli, Gilad Schalit, ambaye wanamapambano wa Hamas walikuwa wamemkamata miaka mitano kabla.

Sinwar, kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Hamas, anapinga mapatano ya maelewano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wapiganaji wa Brigedi ya Ezzedine Qassam

Ukanda wa Ghaza uko chini ya mzingiro wa kinyama wa utawala haramu wa Israel tokea mwaka 2007. Aidha utawala haramu wa Israel umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ukanda wa Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelefu ya Wapalestina wameshauawa, wengi wao wakiwa ni raia hasa wanawake na watoto wadogo.

Tags