Saudia yanunua idadi kubwa ya 'silaha za kichokozi'
Wataalamu wa kijeshi wamefichua kuwa, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Kiarabu zinazopata himaya ya nchi za Magharibi zimenunua idadi kubwa ya silaha za 'kichokozi' na zenye uwezo wa kutumika kuhujumu masafa ya mbali.
Wataalamu wa kijeshi wa Taasisi ya IHS Jane's wamesema Saudia imenunua silaha za kuimarisha uwezo wa kuhujumu wa ndege za kivita kama vile makombora erevu ya anga kwa nchi kavu na ndege kubwa za kubeba mafuta ili ziweze kuongeza mafuta ya ndege za kivita zikiwa angani na hivyo kurefusha muda wa kuruka ndege hizo.
Taasisi ya IHS Jane's yenye makao yake London imesema Saudia pia inalenga kununua ndege mpya za kivita za Panavia Tornado na Eurofighter Typhoon kutoka Uingereza. Saudia vilevile inalenga kuimarisha uwezo wa 'kichokozi' wa jeshi lake la majini. Taarifa hiyo imesema bajeti ya kijeshi ya Saudi Arabia inatazamiwa kufika dola bilioni 180 ifikapo mwaka 2020.
Mwaka 2016 Saudia ilikuwa ya nne kwa ukubwa wa bajeti ya kijeshi duniani baada ya Marekani, China na India. Mtaalamu wa IHS Reed Foster anasema nchi za Kiarabu ambazo ni waitifaki wa Marekani na Uingereza zinanunua silaha ambazo zitaziwezesha kutekeleza oparesheni ya kuhujumu nje ya mipaka yao katika hali ambayo huko nyuma nchi hizo zilikuwa zikinunua silaha za kujihami tu.
Saudi Arabia ilianzisha vita dhidi ya Yemen Machi 2015 kwa lengo la kuirejesha serikali kibaraka nchini humo vita ambavyo vimepelekea Wayemen karibu 12 elfu kuuawa. Hata hivyo pamoja kuwa inamiliki idadi kubwa ya silaha na kupata himaya ya nchi za Magharibi na utawala haramu wa Israel, Saudia imeshindwa kufikia malengo yake na sasa imekwama katika kinamasi nchini Yemen.
Hali kadhalika Saudia imetuma wanajeshi wake katika nchi jirani ya Bahrain kukandamiza mwamko wa Kiislamu wa wananchi ulioanza mwaka 2011 lakini hadi sasa mwamko huo si tu kuwa haujazimwa bali umezidi kushika kasi.