Abbas afanya mazungumzo na spika wa zamani wa Knesset
(last modified Sat, 18 Feb 2017 08:19:02 GMT )
Feb 18, 2017 08:19 UTC
  • Abbas afanya mazungumzo na spika wa zamani wa Knesset

Rais wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amekutana na kufanya mazungumzo na spika wa zamani wa Bunge la Israel, Knesset katika mji wa Ramallah siku chache tu baada ya Waziri wa Utamaduni wa utawala huo haramu kutoa wito wa kufutwa kikamilifu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) katika Ukanda wa Gaza.

Mahmoud Abbas Alkhamisi iliyopita alikutana na kufanya mazungumzo na Abraham Burg kwa matumaini ya kuanzishwa tena mazungumzo ya PLO na Israel ambayo yalisimama tangu miaka miwili iliyopita.

Katika kipindi cha miaka hiyo miwili, Israel iliendelea kutenda jinai za kutisha dhidi ya raia wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuua shahidi raia wasio na hatia, kufanya mashambulizi ya ugaidi wa silaha za kibiolojia na kemikali (bioterrorism), ukatili na kuwatesa mahabusi wa Kipalestina.

Watoto wa Gaza waliouawa na mashambulizi ya Isarel

Mahmoud Abbas anafuatilia suala la kuanzishwa tena mazungumzo eti ya amani na utawala katili wa Israel licha ya kwamba, hata serikali iliyoondoka madarakani ya Marekani, muungaji mkono mkubwa wa Israel, ilishindwa kuhuisha tena mazungumzo hayo tangu mwaka 2014. Nukta nyingine muhimu ni kuwa, mkutano ulioitishwa Paris Januari mwaka huu wa 2017 kwa ajili ya mgogoro wa Palestina na utawala ghasibu wa Israel pia ulimalizika bila ya kufikia matunda yoyote.

Katika upande wa pili Mahmoud Abbas anafanya mazungumzo na viongozi wa zamani na sasa wa Israel wakati mapambano ya Intifadha ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiendelea kushika kasi zaidi.

Abbas anasahau au anajisahaulisha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha ukatili na njama zake za kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya makundi mbalimbali ya Palestina. Njama za hivi karibuni zaidi ni zile za Waziri wa Vita wa Isarel, Avigdor Lieberman ambaye amedai kuwa, Hamas ndiyo sababu ya matatizo ya kiuchumi ya Ukanda wa Gaza na kusema iwapo wakazi wa eneo hilo wataiondoa madarakani Hamas, Israel itaifanya Gaza kuwa "Singapore ya pili"! 

Avigdor Lieberman

Ukweli ni kuwa, utawala haramu wa Israel ambao katika miezi ya hivi karibuni umechukua hatua kadhaa za kukabiliana na stratijia za Hamas, unapanga mikakati ya kuangamiza kabisa uwezo wa kujeshi na wa kujilinda wa harakati hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina. Kutimia kwa lengo hilo kutairahisishia Israel kudumisha ukatili na jinai zake za kutisha dhidi ya Wapalestina bila ya upinzani wala jibu lolote. 

Utawala kikatili wa Israel unaamini kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayoongozwa na Mahmoud Abbas si tishio kwa utawala huo; kwa msingi huo, inafanya kila iwezalo kuzusha hitilafu kati ya harakati mbalimbali za mapambano za Palestina kupitia njia ya kuinyooshea kidole Hamas na kuiarifisha kuwa ndiyo sababu ya hali mbaya hususan katika Ukanda wa Gaza.  

Tags