Wanajeshi wa Yemen waangamiza mamluki, kusini mwa Saudia
Jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo vimeshambulia kwa kombora kituo cha komandi ya kijeshi cha Saudi Arabia katika eneo la Asir la kusini mwa Saudia na kuangamiza mamluki kadhaa wa nchi hiyo.
Shirika la habari la Tasnim limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen jana viliishambulia pia kwa mizinga kambi ya kijeshi ya al Misyal huko Najran, kusini mwa Saudi Arabia.
Mamluki wengine wanne wa Saudi Arabia wameuliwa na jeshi la Yemen katika eneo la al Tabba al Hamra, kaskazini mwa mkoa wa San'a nchini Yemen.
Wakati huo huo jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vimefanikiwa kuzima shambulio la wanajeshi wa Saudi Arabia na mamluki wao waliotaka kuteka maeneo ya jeshi la Yemen katika eneo la Asir. Maluki 30 wa Saudi Arabia wameangamizwa kwenye operesheni hiyo.
Itakumbukwa kuwa, Saudi Arabia ilianza mashambulizi ya kivamizi dhidi ya wananchi wa Yemen mwaka 2015 na hadi hivi imeshafanya jinai zisizoelezeka dhidi ya wananchi na kila kitu chao huko Yemen.
Mwanzoni mwa uvamizi wake, Saudia ilidai kuwa ina lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdu Rabuh Mansour Hadi na kuimaliza harakati ya wananchi ya Ansarullah, lakini hadi leo hii imeshindwa kufikia lengo hilo. Zaidi ya wananchi 11 elfu wa Yemen wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huyo wa Saudia na kundi lake nchini Yemen.