Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25654-safari_ya_waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_saudia_nchini_iraq
Jumamosi ya jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia aliwasili mjini Baghdad kwa ajili ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2017 04:54 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia nchini Iraq

Jumamosi ya jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia aliwasili mjini Baghdad kwa ajili ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Iraq.

Baada ya Adel al-Jubeir kuwasili mjini Baghdad adhuhuri ya jana, alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa Saudi Arabia kufanya safari nchini Iraq tangu mwaka 2003. Katika mkutano huo pande mbili hizo, zilijadiliana kuhusu mabadiliko ya eneo la Mashariki ya Kati na suala la kuimarisha mahusiano ya pande mbili sambamba na kuondolewa vizuizi vilivyopo kwa ajili ya kuinua mahusiano baina ya pande hizo.

Baada ya Adel al-Jubeir kuwasili mjini Baghdad

Itafahamika kuwa, mahusiano baina ya Saudia na Iraq yalikuwa na panda shuka katika kipindi cha dikteta Saddam Hussein na kabla ya kuondolewa utawala wa Baath, ambapo nchi mbili hizo zilifikia kuitana maadui wakubwa. Tangu mwaka 2003 sambamba na kujiri mabadiliko katika muundo wa utawala nchini Iraq, kuliandaliwa fursa mpya kwa ajili ya Baghdad na Riyadh kuweza kupiga hatua katika njia ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina yao. Mwaka 1990, Saudia ilifunga ubalozi wake nchini Iraq, baada ya jeshi la nchi hiyo kushambulia Kuwait. Hata hivyo uhusiano  wa kidiplomasia baina ya Saudia na Iraq ulifunguliwa tena kwa ngazi ya wawakilishi wa maslahi tu hapo mwaka 2004 yaani baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Saddam.

Nembo ya Harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq inayoitia tumbojoto Saudia

Uhusiano huo wa udiplomasia kwa ngazi ya uwakilishi uliendelea hadi Disemba mwaka 2015, ambapo Riyadh iliamua kufungua ubalozi kamili mjini Baghdad. Hata hivyo mienendo ya kiuhasama, uingiliaji wa balozi wa Saudia katika mambo ya ndani ya Iraq na kadhalika uungaji mkono wa wazi na wa siri wa balozi huyo kwa makundi ya kigaidi na ukufurishaji kupitia siasa ghalati za Riyadh, ilisambaratisha fursa chanya za kupanuliwa mahusiano ya nchi mbili hizo.

Baada ya ubaridi kutawala kwa mara nyingine mahusiano ya Iraq na Saudi Arabia, Riyadh na kupitia siasa zake za kiuhasama dhidi ya Baghdad, ikaamua kupunguza mahusiano hayo ya udiplomasia na kufikia ngazi ya chini ya maafisa wa ubalozi. Radiamali ya raia wa Iraq kuhusiana na siasa za Riyadh katika kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao na kadhalika upinzani wao juu ya teuzi za maafisa wenye historia tata kulikofanywa na Saudia, yote hayo yanabainisha kwamba kamwe Iraq haiwezi kuwa eneo la kupenyezwa  siasa za Aal-Saud. Hii ni kwa kuwa maafisa wa udiplomasia wa Saudia nchini Iraq, walihusika na uenezaji wa propaganda chafu dhidi ya harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi na kueneza habari za uongo na tuhuma mbalimbali kwa lengo la kudhoofisha nafasi ya wapiganaji wa harakati hiyo nchini humo. Ni kutokana na hayo ndipo Wairaq wakawatambua maafisa hao wa udiplomasia wa Saudi Arabia kuwa na mahusiano ya karibu na wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS.) Ukweli ni kwamba kufunguliwa ubalozi wa Saudia nchini Iraq baada ya kupita miaka 25, kinyume na matarajio ya wengi hakukuwa na maslahi kwa Wairaq na badala yake uingiliaji wa viongozi wa Saudia dhidi ya nchi yao uliibua hasira za asilimia kubwa ya raia wa nchi hiyo. Hii ni kusema kuwa, katika kipindi hicho siasa za kigeni za Aal-Saud zilijikita tu juu ya uungaji mkono kwa wapinzani dhidi ya serikali ya kisheria ya Iraq, kukochea serikali ya eneo la Kurdistan dhidi ya serikali kuu ya Baghdad, kupenyeza sumu ya fitina na tofauti baina ya koo za Kisuni na kuwachochea viongozi wa koo hizo kufanya upinzani dhidi ya serikali na kuunga mkono kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh.

Sehemu ya jinai za magaidi hao wanaopata himaya ya Saudia, wakiwachoma moto bila ya huruma watoto wadogo

Mienendo hiyo ilisababisha Wairaq kuitaka serikali yao kuangalia upya namna ya kuamiliana na Saudia sambamba na kuchukua hatua imara katika kukabiliana na uingiliaji wa Saudia ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Katika kipindi ambacho operesheni za jeshi kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi dhidi ya wanachama wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) zilipoingia hatua ya yake ya mwisho, Saudia iliingilia operesheni hizo kwa lengo la kuwasaidia vibaraka wake  kunako kushindwa kikamilifu.

Jeshi la Iraq likizidi kupata ushindi dhidi ya magaidi wa Kiwahabi wa Daesh

Alaa kulli haal! Safari ya papara ya Adel al-Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia mjini Baghdad na kudai kutaka urafiki na kufungua mlango wa mahusiano na Iraq, ni sehemu ya njama mpya ya utawala wa Aal-Saud kwa ajili ya kufikia malengo yake machafu katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo Iraq yenyewe. Suala hilo linatoa udharura wa viongozi wa Baghdad kuwa macho kunako harakati hizo za Saudia dhidi ya nchi yao.