VIDEO: Israel yatuma majasusi nchini Syria
Kikosi maalumu cha jeshi la Israel kimeingia kwenye ardhi ya Syria kwa ajili ya kufanya ujasusi.
Shirika la habari la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran (ISNA) limeinukuu Kanali ya Pili ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni ikifichua habari hiyo leo kuwa, kikosi maalumu cha majasusi wa Israel kimeingia katika ardhi ya Syria kwa kupitia maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1948.
Mwandishi wa Kanali hiyo ya Pili ya Israel, Danny Kushmaro ambaye alifuatana na wanajeshi hao anasema, majasusi wa Israel waliingia kwa miguu hadi kwenye kijiji kilichoko umbali na nusu kilomita ndani ya ardhi ya Syria.
Kabla ya hapo, Waziri wa Vita wa Israel alikiri kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unashirikiana kwa karibu na magenge ya kigaidi yanayofanya mauaji dhidi ya raia na maafisa usalama wa serikali ya Syria.
Kabla ya hapo pia, jeshi la Lebanon lilitangaza kuwa, limegundua kifaa cha kijasusi cha utawala wa Kizayuni kilichokuwa kimetegwa katika milima ya al Barouk iliyoko baina ya kijiji cha al Barouk na Ain Zahlan huko kusini mwa Lebanon, na kukitegua.
Si hayo tu, lakini pia wanajeshi wa Israel wamekuwa wakiwapa huduma za afya na kuwatibu magaidi wanaojeruhiwa katika mashambulizi yao dhidi ya maafisa usalama wa serikali ya Syria.
Mwezi Septemba mwaka jana pia, mbunge wa Israel, Akram Hasson alisema kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni aliwasaidia magaidi wa Jabhat an Nusra katika mashambulizi yao dhidi ya kijiji cha Khadr cha watu wa kabila la Druze.