Wairaq: Ni kosa kubwa kuwaamini watawala wa kigaidi wa Saudia
Sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Adel al-Jubeir kufanya safari nchini Iraq na kukutana na viongozi wa nchi hiyo ambapo ametaka kuimarishwa mahusiano ya pande mbili, Wairaq wameitaja safari ya waziri huyo wa Saudia kuwa ni njama chafu dhidi ya nchi yao.
Hassan Salim, mmoja wa wawakilishi katika bunge la Iraq amesema kuwa, utawala wa Aal-Saud ni chombo cha utawala wa Kizayuni wa Israel.
Salim ambaye ni mwanachama wa mrengo wa Swadiqun katika bunge la Iraq amesema kuwa, Al-Jubeir na utawala wa kigaidi wa Aal-Saud kwa ujumla ni vibaraka wa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kufanya mauaji dhidi ya watu wa mataifa ya Kiislamu na kwamba kuwadhania dhana nzuri au kuwaamini watawala hao ni kosa kubwa. Ameongeza kuwa, utawala wa Saudi Arabia ni utawala uliotapakaa damu za jinai mbalimbali dhidi ya mataifa ya Kiarabu.
Hassan Salim amesema kuwa, mauji ya kutisha dhidi ya Wairaq, Wayemen na Wasyria ni ushahidi thabiti wa namna ambavyo mikono ya watawala wa Aal-Saud ilivyotapakaa damu sambamba na kuunga mkono kwake makundi ya kigaidi. Kwa mujibu wa mwakilishi huyo katika bunge la Iraq, safari ya Adel al-Jubeir nchini humo ni katika mfululizo wa utekelezaji wa njama mpya za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Baghdad.
Kwa ajili hiyo amewataka viongozi wa serikali ya Iraq kuwa macho kutokana na njama hizo na kwamba ikiwa kweli Saudia imekusudia kuanzisha uhusiano mwema na nchi yao, lazima ihitimishe kwanza uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi nchini humo. Al-Jubeir alifanya safari nchini Iraq Jumamosi ya tarehe 25 mwezi huu. Hata hivyo wanasiasa wengi wa nchi hiyo na vyombo mbalimbali vya habari vimekosoa vikali safari hiyo.