WFP yaeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya Iraq
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu inayozikabili familia za Wairaqi magharibi mwa mji wa Mosul nchini humo.
Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa taasisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya familia mbalimbali za Wairaqi huko magharibi mwa mji wa Mosul na kwamba zaidi ya watu 750,000 wakazi wa mji huo wana hali ngumu. WFP hivi karibuni ilikadiria kuwa, bidhaa za chakula katika eneo hilo zimepungua kutokana na kukatwa kwa njia zote za ufikishaji wa chakula katika mji huo. Mpango wa Chakula Duniani pia umesisitiza kuwa kwa kuzingatia kuongezeka mapigano, wananchi wana hofu na woga wa kuziacha nyumba zao na kwamba suala hilo linasababisha kukwama zaidi juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kuwadhaminia raia mahitaji ya chakula.
Sally Haydock Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) huko Iraq amezitolea wito pande zinazozozana katika mji wa Mosul kuruhusu kufikishwa haraka iwezekanavyo misaada ya kibinadamu kwa familia zote zinazohitajia.