Hamas yapinga fikra ya kupelekwa askari wa kimataifa Ukanda wa Gaza
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa harakati hiyo haitakubali harakati yoyote ya kutuma askari wa kimataifa katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Abdul Latif al Qanu'u amesisitiza udharura wa kukomeshwa uvamizi wa Israel na mzingiro wa Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, hatua yoyote ya kutaka kutuma askari wa kimataifa katika eneo hilo inatambuliwa kuwa ni kuingilia mambo ya ndani ya Gaza na kuvuruga kadhia ya Palestina.
Al Qanu'u ameongeza kuwa, kutumwa askari wa kimataifa katika Ukanda wa Gaza ni sawa na kutumwa askari vamizi wa kimataifa katika eneo hilo kwa ajili ya kuusaidia utawala haramu wa Israel.
Katika safari yake ya hivi karibuni nchini Australia, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alizungumzia suala la Israel kudhibiti kikamilifu eneo la Ukingo wa Magharibi, kubana shughuli za Mamlaka ya ndani ya Palestina na kutumwa askari wa kimataifa katika Ukanda wa Gaza.
Hata hivyo wapambe wa Netanyahu hadi sasa hawajawasilisha rasmi mpango huo kwa kuchelea hitilafu ndani ya baraza la mawaziri la serikali ya mseto ya Israel.