Maelfu ya Wasyria wamekuwa wakimbizi kaskazini mwa nchi
Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) limeripoti kuwa maelfu ya raia wa Syria wamekuwa wakimbizi katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
OCHA imesema leo kuwa watu elfu 66 kutoka miji ya al Bab na Taduf katika mkoa wa Halab yaani Aleppo kaskazini mwa Syria wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na kuwepo magaidi. Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limeashiria namna Wasyria elfu 40 katika mji wa al Bab na wengine elfu 26 katika mji wa Taduf walivyolazimika kuyahama makazi yao kwa kuhofia mashambulizi ya kigaidi na kuongeza kuwa, raia elfu 39 na 766 wakazi wa mji wa al Bab wamekimbilia katika maeneo ambako kungali kuna makundi ya wapinzani wanaobeba silaha dhidi ya serikali.
Shirika hilo limeongeza kuwa baadhi ya raia wa Syria wameshindwa kutoka katika maeneo ambayo yanashikiliwa na makundi yenye silaha kutokana na magaidi kutega mabomu ya ardhini na mada za milipuko katika njia za kupitia. Magaidi wangali wanaendesha hujuma katika maeneo ya kaskazini mwa Syria ikiwa ni pamoja na kuvurumisha makombora, kutega mabomu kwa wingi na kuwaua wananchi wa Syria wasio na hatia baada ya kupata pigo kubwa kwa jeshi la nchi hiyo na vikosi vya kujitolea vya wananchi.