Wasiwasi wa kutumia ISIS silaha zaidi za kemikali nchini Iraq
Shirika la Msalaba Mwekundu limetoa taarifa ya kulaani mashambulizi ya silaha za kemikali ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) dhidi ya raia wasio na ulinzi wa mji wa Mosul huko Iraq.
Aidha shirika hilo limesema liko tayari kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwasaidia watu waliojeruhiwa katika hujuma hiyo. Katika ripoti hiyo, Lise Grande, mratibu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinaadamu nchini Iraq, amesema kuwa shambulio hilo la silaha za kemikali mjini Mosul ni la kutisha na kuongezwa kwamba, hakuna utetezi wowote unaoweza kuhalalisha kutumiwa silaha hizo haramu. Hii ni katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti habari ya kujiri mashambulizi ya silaha za kemikali huko mashariki mwa mji wa Mosul nchini Iraq. Sa'adun Khalid al-Ramadhan, mmoja wa makamanda wa kikosi cha radiamali ya haraka katika jeshi la Iraq amenukuliwa akisema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh limevurumisha maroketi ya Katyusha yenye gesi ya sumu katika maeneo ya raia mjini Mosul.
Kabla ya hapo pia, Shirika la Habari la Business Wire kwa kutegemea ripoti ya kituo cha utafiti cha IHS chenye makao yake nchini Marekani, lilitangaza kuwa, tangu mwaka 2014 kundi la kigaidi la Daesh, limetumia mara 71 silaha za kemikali nchini Iraq na Syria tena katika maeneo ya raia. Kwa mujibu wa taarifa za kiintelejensia za vyombo vya usalama nchini Iraq, Uturuki ilinunua silaha hizo za kemikali kwa fedha za Saudia na Qatar, kutoka Ukraine na baadhi ya nchi za Magharibi, na kisha kulipa silaha hizo kundi hilo la kigaidi la Daesh. Hatua za serikali za Magharibi katika kuyapa makundi ya kigaidi silaha za maangamizi sambamba na kuyapatia vifaa vya kuundia silaha hizo haramu, ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba yote ya kimataifa.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba, ili kuzuia kushindwa kikamilifu huko mjini Mosul, kundi la Daesh limeamua kutumia silaha za kemikali. Kwa kuzingatia kushindwa mtawalia na kuanza kusambaratika kikamilifu kundi hilo la kigaidi nchini Iraq, kuna uwezekano mmkubwa genge hilo likapanua wigo wa matumizi ya silaha hatari za kemikali. Lengo la kundi hilo la Daesh katika kutumia silaha hizo za kemikali ni kuzitia hofu nyoyo za raia wa Iraq ili kuwafanya waendelee kutii amri za genge hilo. Asasi za kutetea haki za binaadamu sambamba na kukosoa mienendo ya magaidi wanaobeba silaha nchini Iraq na Syria, zimesisitiza kwamba makundi hayo yanafanya kila liwezekanalo kuzuia kukombolewa kikamilifu maeneo yanayoyadhibiti.
Mwaka 2014 kundi la wakufurishaji la Daesh kupitia uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na Kiarabu, ikiwemo Saudia, Uturuki na Qatar, lilianzisha mashambulizi nchini Iraq na kudhibiti eneo kubwa la kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo. Katika harakati hizo genge hilo lilifanya jinai zisizohesabika ikiwemo kutumia silaha za kemikali katika maeneo ya raia. Nukta ya kufaa kuzingatiwa hapa ni kuwa, katika kujaribu kupotosha fikra za walio wengi, makundi ya kigaidi na kwa uungaji mkono kamili wa madola ya Magharibi na waitifaki wake wakiwemo viongozi wa baadhi ya nchi za Kiarabu, sambamba na kutenda jinai kubwa dhidi ya binaadamu nchini Iraq na Syria, yamekuwa yakijaribu kuzitwisha serikali za nchi hizo tuhuma hizo. Kutokana na kundi la Daesh na makundi mengine mfano wake kukariri mara kadhaa katika utumiaji wa silaha hizo za maangamizi, umefika wakati sasa wa kuundwa nguvu ya pamoja ya kupambana na hatari ya makundi hayo. Kadiri unavyokuwepo uzembe katika uwanja huo, ndivyo madhara ya jinai za magenge hayo nchini Iraq na Syria yanavyozidi kuwa makubwa na kuwa jinai ya kimataifa.