Hakuna anayesalimika na mashambulizi ya magaidi nchini Misri
(last modified Tue, 07 Mar 2017 04:31:50 GMT )
Mar 07, 2017 04:31 UTC
  • Hakuna anayesalimika na mashambulizi ya magaidi nchini Misri

Makumi ya familia za Wakristo zimelazimika kukimbia makazi yao katika mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri kutokana na mashambulizi ya watu wenye silaha.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Munir Abul Khair, mwakilishi wa Wizara ya Masuala ya Kijamii ya Misri katika mkoa wa Sinai Kaskazini akisema kuwa, familia 258 za Wakristo zimekimbia mashambulizi ya magenge yenye silaha na kukimbilia kwenye mikoa 13 yenye Waislamu wengi nchini Misri.

Wakristo wa Kibt wakiwa kanisani nchini Misri

 

Abul Khair ameongeza kuwa, vikosi vya kulinda usalama vya Misri vimeweka ulinzi mkali katika maeneo yenye makanisa ili kuwalinda raia Wakristo wa nchi hiyo.

Wiki iliyopita, watu wenye silaha waliua Wakristo 7 wa Kibti, kaskazini mwa Misri na kupelekea idadi kubwa wa jamii za Wakristo wa mkoa wa Sinai Kaskazini kukimbilia maeneo yenye Waislamu wengi kuomba hifadhi.

Genge la kigaidi la  Wilaya ya Sinai, tawi la kundi la wakufurishaji la Daesh katika mkoa wa Sinai Kaskazini huko Misri, limetangaza kuhusika na mauaji hayo.

Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri

 

Wiki iliyopita, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri alipinga pendekezo la kuondolewa wakazi wote wa mji wa al Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini, kutokana na kushadidi mashambulizi ya magaidi, kaskazini mwa Misri.

Hivi karibuni pia Rais wa Misri alisema kuwa, mashambulizi ya makundi yenye silaha yanafanyika kwa nia ya kueneza fitna na kuwagombanisha wananchi wa Misri na baadaye kuisingizia serikali na kujaribu kuonesha kuwa imeshindwa kuwalinda wananchi wakiwemo Wakristo.

Tags