Wapinzani Maldives wapinga Saudia kuuziwa visiwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26238-wapinzani_maldives_wapinga_saudia_kuuziwa_visiwa
Vyama vya upinzani nchini Maldives vimepinga safari ya mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia nchini humo baada ya kuvuja ripoti kuwa anataka kununua sehemu kubwa ya visiwa vya nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Asia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2017 10:54 UTC
  • Wapinzani Maldives wapinga Saudia kuuziwa visiwa

Vyama vya upinzani nchini Maldives vimepinga safari ya mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia nchini humo baada ya kuvuja ripoti kuwa anataka kununua sehemu kubwa ya visiwa vya nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Asia.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje ya Maldives, Ahmed Naseem wa chama cha upinzani cha MUO amesema watawafahamisha watawala wa Saudia kuwa  Wamaldives hawatakubali kuiuza ardhi ya nchi yao. Ameonya kuwa kutafanyika maandamano katika mji mkuu, Malé kupinga uuzaji huo wa mabilioni ya dola wa ardhi ya Maldives. 

Kuna taarifa kuwa, utawala wa Saudia unalenga kununua visiwa 28 vidogo vya matumbawe katika eneo la Faafu ambavyo wamepanga kuvinunua kwa dola bilioni 10. Maldives yenyewe ni nchi ndogo katika Bahari ya Hindi na visiwa vyake vingi vinaripotiwa kuangamia kutokana na kuongezeka kiwango cha maji baharini. Wapinzani wanaituhumu serikali kuwa inawakandamiza wapinzani kabla ya safari ya mtawala huyo wa Saudi Arabia ambaye yuko safarini mashariki mwa Asia.

Moja kati ya visiwa vya matumbawe nchini Maldives

Safari ya Mfalme Salman ilianzia Malaysia kisha Indonesoa na Brunei na anatazamiwa kuelekea China na Japan kabla ya kumalizia Visiwani Maldives.

Safari ya Mfalme Salman mashariki mwa Asia imeandamana na israfu na ubadhirifu mkubwa na ndege zake zimebeba mizigo inayokadiriwa kufikia tani karibu 500. Ujumbe wa watu 600 wakiwemo wanamfalme 25, mamia ya maafisa usalama, mawaziri 10, wahudumu na magari kadhaa ya kifahari yanaandamana na Mfalme huyo.