Vipaza Sauti vya adhana katika nyumba Wapalestina kupinga amri ya Israel
Idadi kubwa ya Wapalestina wameweka vipaza sauti vya adhana katika paa za nyumba zao kama njia ya kuonyesha upinzani wao kwa sheria ya Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel kupiga marufuku ya adhana katika mji wa Quds na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Duru za habari zinaarifu kuwa, Wapalestina wameweka vipaza sauti vya adhana katika paa za nyumba zao huku wakisisitiza kuwa, sauti ya adhana kamwe haitazimika katika mji wa Quds.
Morsey Abo Mokh, meya wa mji wa Baqa al-Gharbiyye katika makazi ya Warabu wilaya ya Haifa ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ameamuru kuwa kuadhiniwe kupitia vipaza sauti vilivyowekwa juu ya jengo la manispaa.
Kwa upande wake Farhan Haq, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani hatua hiyo ya Israel kupiga marufuku adhana. Amesema Israel inapaswa kuheshimu haki za kidini za Wapalestina.
Siku ya Jumatano, Bunge la Utawala wa Kizayuni wa Israel, Knesset, lilipitisha rasimu ya sheria ya kupiga marufuku adhana katika misikiti yote iliyopo katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Kwa muda mrefu sasa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakitekeleza njama ya kufuta utambulisho wa Kiislamu na Ukristo katika Quds tukufu na badala yake kulipa eneo hilo utambulisho bandia wa Kizayuni.