Wayemen wataka kuundwe kamati ya kuchunguza jinai za Saudia nchini mwao
Serikali ya Yemen imetaka kuundwe kamati huru ya kimataifa ya kuchunguza jinai za Saudi Arabia nchini humo.
Shirika la habari la Yemen SABA limeripoti habari hiyo na kumnukuu Hisham Sharaf Abdullah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya nchi hiyo akisema jana Jumatano kwamba serikali hiyo imemtaka Zeid bin Ra’ad Zeid al-Hussein, kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuunda kamati huru ya kimataifa ya kuchunguza jinai za Saudi Arabia nchini Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen amesisitiza kuwa, Saudi Arabia inatumia vibaya uwanachama wake katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na inalikwamisha baraza hilo kuchukua hatua linazotaka.
Saudia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na kwa uungaji mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen tangu mwezi Machi 2015 hadi hivi sasa. Saudia inadai kuwa lengo lake ni kumrejesha madarakani Abdu Rabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia.
Ukoo wa kifalme wa Aal Saud umefanya jinai kubwa nchini Yemen tangu wakati huo hadi hivi sasa kiasi kwamba umeshaua zaidi ya watu 12 elfu, umeshajeruhi makumi ya maelfu ya wengine na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya Wayemen sambamba na kuharibu kikamilifu miundombinu ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu kama vile mashule, misikiti, mahospitali, viwanja vya ndege, madaraja n.k.