Iran yalaani hujuma ya Marekani katika msikiti nchini Syria
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya ndege za kivita za Marekani kuushambulia kwa mabomu msikiti mmoja katika kitongoji kimoja cha mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria.
Katika taarifa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amesema: "Kushambulia maeneo matukufu na ya kidini kwa lengo lolote lile ni jambo linalolaaniwa na haliwezi kutetetwa hata kidogo."
Siku ya Alhamisi raia wasiopungua 46 waliuawa katika shambulio la anga la jeshi la Marekani lililolenga Msikiti wa Umar ibn Al-Khaṭṭab uliokuwa umejaa waumini ndani yake karibu na mji wa Halab kaskazini mwa Syria. Watu wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa katika shambulio hilo lililofanywa katika kijiji cha al-Jineh kilichopo kilomita 30 magharibi mwa mji wa Halab.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema haitoshi kukiri Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani kuwa msikiti huo ulilengwa lakini si kwa makusudi. Amesema Marekani inapaswa kuwajibika na kuchukua dhima ya jinai hiyo iliyowalenga raia waliokuwa wamemefkia msikitini hapo kwa ajili ya ibada.
Ndege za kivita za Marekani zimekuwa zikitekeleza mashambulizi ndani ya Syria kwa madai ya kuwalenga magaidi lakini badala yake mamia ya raia wasiokuwa na hatai wamekuwa wakilengwa katika hujuma hizo zinazotekelezwa bila ya idhini ya serikali ya Syria.
Wakuu wa Syria wanasema jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kutoa pigo kubwa kwa magaidi ambapo wameshindwa katika maeneo mengi. Pamoja na kuwepo mafanikio hayo, katika miezi ya hivi karibuni ndege za kivita za Marekani zimeiujumu Syria kwa lengo lakuwapa nguvu magaidi na kudhoofisha jeshi na wanamgambo watiifu kwa serikali.