HRW: Daesh imezika mamia ya watu katika kaburi la umati, Mosul
Shirika la kutetea haki za bindamu la Human Rights Watch (HRW) limeripoti kuwa kundi la kigaidi la Daesh limeua mamia ya mahabusi katika mji wa kaskazini mwa Iraq wa Mosul na kuwazika katika kaburi la umati ambalo yumkini likawa kubwa zaidi ya makaburi yote ya umati yaliyogunduliwa nchini Iraq hadi hivi sasa.
HRW imeripoti kuwa watu walioshuhudia wamesema, wahanga waliozikwa katika kaburi hilo ni pamoja na maafisa usalama wa Iraq waliouawa katika kipindi cha kati ya Juni 2014 na Mei mwaka 2015.
Ripoti ya Human Rights Watch imesema wanachama wa kundi la kigaid la Daesh wametega mabomu katika kaburi hilo la umati ili kuua watu wengi zaidi.
Mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati, Lama Fakih, amesema kuwa kaburi hilo la umati ni nembo ya unyama na ukatili wa wanachama wa kundi la Daesh.
Jeshi la Iraq liligundua kaburi hilo mwezi Februari mwaka huu na mashirika ya kutetea haki za binadamu yalifika mahala hapo machi 7 lakini yameshindwa kukagua miili ya watu waliozikwa humo kutokana na hatari ya mabomu ya kutegwa ardhini yaliyowekwa humo na wapiganaji wa Daesh.
Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba kazi ya kuondoa mabomu yote yaliyotegwa na Daesh katika maeneo mbalimbali na makaburi ndani na nje ya mji wa Mosul itagharimu kiasi cha dola milioni 50.