Mazungumzo ya Geneva-5 yaanza rasmi kuhusu mgogoro wa Syria
Mazungumzo rasmi yajulikanayo kwa jina la Geneva-5 yameanza nchini Uswisi kati ya Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria na makundi mengine yanayoshiriki kwenye mazungumzo hayo.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria, Stephen de Mistura ambaye kabla ya kuanza mazungumzo haya alikutana na kufanya mazungumzo mjini Moscow na Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa, masuala manne ambayo yatachunguzwa katika kikao cha Geneva ni katika fremu ya kutekeleza azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama na kwa mujibu wa taarifa ya Geneva. Miongoni mwa masuala ya kimsingi yaliyomo katika azimio nambari 2254 lililopasishwa mwezi Disemba mwaka juzi ni kuanisha ramani ya njia kwa ajili ya mazungumzo ya amani, kufikiwa usitishaji vita kote nchini Syria na kufanyika uchaguzi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini jana alieleza kuwa, kuanza mazungumzo kati ya makundi ya Syria huko Geneva ni hatua muhimu kwa ajili ya kupata njia ya kisiasa ya kuhitimisha hali ya machafukoge huko Syria. Taarifa ya Mogherini imeongeza kuwa, mapigano yameingia katika mwaka wa saba huko Syria na kuongeza kuwa, hali hii inadhihirisha kwamba, hakuna ufumbuzi wa kudumu wa kijeshi kwa mgogoro uliopo huko Syria.
Mkutano wa Geneva -5 kuhusu Syria ulianza jana mjini Geneva, Uswisi kwa kudhuhuriwa na pande zote. Hata hivyo mazungumzo ya mkutano huo yameanza rasmi leo na yanatazamiwa kuendelea kwa kipindi cha siku kumi.