HRW yakosoa shambulio la Saudia dhidi ya wakimbizi wa Kisomali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26932-hrw_yakosoa_shambulio_la_saudia_dhidi_ya_wakimbizi_wa_kisomali
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limelitaja shambulio lililofanywa hivi karibuni na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya boti iliyokuwa imewabeba wakimbizi wa Kisomali karibu na pwani ya Yemen kuwa ni jinai ya kivita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2017 08:10 UTC
  • HRW yakosoa shambulio la Saudia dhidi ya wakimbizi wa Kisomali

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limelitaja shambulio lililofanywa hivi karibuni na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya boti iliyokuwa imewabeba wakimbizi wa Kisomali karibu na pwani ya Yemen kuwa ni jinai ya kivita.

Human Rights Watch leo imetoa taarifa na kutaka kufanyika uchunguzi huru kuhusu shambulio hilo la Saudia dhidi ya wakimbizi wa Kisomalia. HRW pia imetaka kufikishwa kizimbani utawala wa Saudia kwa jinai yake hiyo.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesisitiza pia kuwa Saudi Arabia inafanya uchunguzi wake kuhusu shambulio hilo dhidi ya wakimbizi wa Kisomali katika pwani ya Yemen ili kusafisha taswira yake na kuficha jinai hiyo; uchunguzi ambao hauna thamani yoyote.

Miili ya wakimbizi wa Kisomali waliouliwa na Saudia katika pwani ya Yemen ikiingizwa garini 

Shirika la Human Rights Watch pia limezituhumu serikali za Washington, London na Paris kwa kuendelea kuiuzia silaha serikali ya Riyadh.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita boti moja iliyokuwa imewabeba wakimbizi wa Kisomali ikiwa katika umbali wa maili 30 kutoka pwani ya Yemen ilishambuliwa na meli ya kijeshi ya utawala wa Saudi Arabia. Wakimbizi wa Kisomali wasiopungua 40 waliuawa kwa umati na wengine 80 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo la kikatili.