Hatua chanya za Lebanon katika njia ya kurejesha uthabiti wa kisiasa
Hatua ya nne chanya ya kisiasa nchini Lebanon inasubiri kupitishwa na bunge la nchi hiyo.
Waziri wa Habari wa Lebanon Melhem Ar-Rayashi, ametangaza kuwa bajeti ya serikali ya mwaka huu wa 2017 imeshapitishwa na Baraza la Mawaziri. Ili muswada huo wa serikali kuhusu bajeti ya matumizi ya fedha uweze kuwa sheria unahitaji kupitishwa rasmi na bunge la nchi hiyo.
Tangu mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2016, Lebanon imeanza kushuhudia mchakato ambao hatua kwa hatua unaelekea kurejesha uthabiti wa kisiasa nchini humo. Mfumo wa kisiasa wa Lebanon ni wa Kibunge na rais wa nchi anachaguliwa na bunge. Baada ya kupita karibu miezi 30 ya ombwe la kisiasa la kubaki wazi kiti cha urais, hatimaye tarehe 31 Oktoba mwaka jana bunge la Lebanon lilimchagua Michel Aoun kuwa rais mpya na kuhatimisha moja ya migogoro mirefu zaidi ya kisiasa kuwahi kutokea nchini humo.
Hatua ya pili iliyochukuliwa na vyama na mirengo ya kisiasa ya Lebanon katika kurejesha uthabiti wa kisiasa ilikuwa ni kuafiki kuteuliwa kiongozi wa harakati ya Al-Mustaqbal, Saad Hariri, kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Hatua mbili hizo chanya zilizochukuliwa na vyama vya siasa zilitosha kufanikisha ufikiaji lengo la tatu, yaani kuundwa serikali mpya bila ya kupoteza muda mrefu kwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa badala ya manufaa ya kichama na kimakundi.
Kwa kuundwa Baraza la Mawaziri, suala la bajeti, uchaguzi, mishahara na marupurupu ni mambo ambayo yamepewa kipaumbele katika utendaji wa serikali ya Saad Hariri. Hivi sasa bajeti ya Lebanon imepitishwa na Baraza la Mawaziri katika hali ambayo kwa muda wa miaka 10 nchi hiyo imekuwa ikiendeshwa bila ya kuwepo sheria ya bajeti. Kutokana na muelekeo mmoja ulioonyeshwa katika miezi ya karibuni na mirengo na makundi ya kisiasa ya Lebanon ndani ya bunge la nchi hiyo, kuna matarajio kuwa hatua ya nne chanya kushuhudiwa katika miezi mitano ya karibuni itachukuliwa kwa kupitishwa sheria ya bajeti na bunge hilo.
Endapo bunge la Lebanon litapitisha bajeti ya nchi hiyo, hatua muhimu itakayofuata kutekelezwa na serikali ya Saad Hariri na mirengo ya kisiasa ni kushirikiana pamoja kwa ajili ya kuzifanyia marekebisho sheria za uchaguzi na vilevile kumaliza tatizo sugu la mishahara na marupurupu; ambapo tab'an, hekima na tadbiri inayohitajika kwa ajili ya masuala mawili hayo ni kubwa na nzito zaidi kuliko ya upitishaji bajeti. Kwa upande mmoja sheria za uchaguzi zina uhusiano wa moja kwa moja na mgawanyo wa madaraka hususan katika bunge, jambo ambalo lina umuhimu pia kwa makundi ya kisiasa ya Lebanon; na kwa upande mwengine mishahara na marupurupu inahitaji uwezo na nguvu za kiuchumi. Tatizo sugu la mishahara na marupurupu ambalo linatajwa katika vyombo vya habari vya Lebanon kama "mlolongo wa wadhifa na nyadhifa" lina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya matabaka mengi ya raia wa Lebanon, kwa sababu licha ya kuongezeka bei za bidhaa na ughali wa maisha, kwa muda wa karibu miaka 20 sasa wafanyakazi wa sekta ya umma hawajapewa nyongeza ya maana ya mishahara. Hali hiyo imezidisha malalamiko na manung'uniko ya wananchi kutokana na hali yao ya maisha.
Pamoja na yote hayo, suala muhimu zaidi la kuzingatiwa kwa sasa kuhusiana na Lebanon ni kwamba, kwa mashauriano na uratibu uliofanywa na mirengo ya kisiasa, nchi hiyo inapiga hatua katika njia ya kuimarisha uthabiti na usalama wake wa kisiasa na kijamii…/