Chama cha Sinn Féin chataka Uingereza isiiuzie Saudia silaha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27160-chama_cha_sinn_féin_chataka_uingereza_isiiuzie_saudia_silaha
Chama cha Sinn Féin cha Ireland Kaskazini nchini Uingereza kimetoa taarifa kikitaka serikali ya nchi hiyo isitishe mara moja uuzaji silaha kwa utawala wa Saudi Arabia.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 01, 2017 23:50 UTC
  • Chama cha Sinn Féin  chataka Uingereza isiiuzie Saudia silaha

Chama cha Sinn Féin cha Ireland Kaskazini nchini Uingereza kimetoa taarifa kikitaka serikali ya nchi hiyo isitishe mara moja uuzaji silaha kwa utawala wa Saudi Arabia.

Katika taarifa ya chama hicho katika  kongamano la 'Sera za Saudia katika eneo lenye migogoro' ambalo limefanyika London, chama cha Sinn Féin  kimebainisha wasiwasi wake kuhusu hujuma za kijeshi za Saudia Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati. Taarifa hiyo imesema Saudia inatekeleza oparesheni za kinyama katika nchi kama vile Syria, Iraq, Misri, Libya, Yemen na Bahrain. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, katika hujuma ya miaka miwili ya Saudia nchini Yemen maelefu wamepoteza maisha na idadi kubwa ya mahospitali, shule na viwanda vimelengwa kwa mabaomu ya Saudia na hivyo kuibua mgogoro mkubwa wa kibinadamu Yemen.

Aidha taarifa ya Sinn Féin  imesema utawala wa Aal Saud ni wa kidikteta na wa kikabila na kwamba utawala huo wa Aal Saud pia unahusika katika kukandamizwa mwamko wa watu wa Bahrain.

Saudi Arabia, kwa himaya ya Marekani, Uingereza na Israel, inatekeleza kila aina ya jinai dhidi ya raia wa Yemen ikiwa ni pamoja na kutumia silaha zilizopigwa marufuku hasa mabomu ya vishada (cluster bombs) na mabomu ya phosphoraus ambayo yanatumiwa kuwaangamiza kwa umati raia wa Yemen.

Uharibifu wa Saudia nchini Yemen

Karibu maeneo yote ya Yemen yameshalengwa kwa mabomu ya Saudia ambapo maeneo yaliyolengwa ni yenye miundomsingi ya madaraja, barabara, shule, mahospitali na misikiti.

Yemen imepata hasara ya mabilioni ya dola kutokana na hujuma za Saudia dhidi ya miundombinu yake kiasi kwamba itachukua makumi ya miaka kuikarabati upya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Saudia Arabia, ilianzisha hujuma zake dhidi ya Yemen Machi 26 mwaka 2015 na hivi sasa mbali na kusababisha hasara kubwa kwa miundombinu, hujuma hiyo imepelekea zaidi ya watu 12,000 kupoteza maisha wengi wakiwa ni raia hasa wanawake na watoto.