Iraq yasisitiza, kuna tofauti kubwa na za kimsingi na Saudi Arabia
Waziri Mkuu wa Iraq amesema kwamba hitilafu zilizopo baina ya Baghdad na Riyadh ni za muda mrefu na kuongeza kuwa, Wairaq wanaitambua Saudi Arabia kuwa inahusika katika mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika nchini humo.
Haider al-Abadi, amesema kuwa, watu wengi wanaofanya mashambulizi ya kigaidi na kujilipua kwa mabomu nchini Iraq ni raia wa Saudia.
Tangu mwaka 2014 kundi la kigaidi la Daesh na kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na Kiarabu ikiwemo Saudia, liliyafanya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq kuwa uwanja wa mapigano yaliyoambatana na jinai kubwa na za kutisha dhidi ya wakazi wa maeneo hayo. Hatua ya Saudia ya kueneza fikra za Uwahabi wa kufurutu ada ambao ndio chanzo cha kuibuka na kupanuka makundi ya kigaidi na ukufurishaji kama vile Daesh na al-Qaidah, ni suala ambalo limezishughulisha fikra za watu katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla, kiasi kwamba hivi sasa walimwengu wote wanautambua utawala wa Aal-Saud kuwa ni utawala wa kigaidi.
Hatua na vitendo vya Saudia pia ni ishara ya kuendelea mienendo ya chuki dhidi ya taifa la Iraq. Itafahamika kuwa, uhusiano wa Iraq na Saudia ulikumbwa na misukosuko mingi katika kipindi cha utawala wa Saddam Hussein na kabla ya utawala wa Baath ambapo nchi mbili zilikuwa zikitambuana kuwa maadui. Tangu mwaka 2003 ambapo Iraq ilikumbwa na mabadiliko ya kiutawala, kuliandaliwa fursa mpya baina ya Baghdad na Riyadh kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia. Mwaka 1990 wakati jeshi la Saddam lilipoishambulia Kuwait, Saudia ilifunga ubalozi wake nchini Iraq.
Hata hivyo mwaka mmoja baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Saddam hapo mwaka 2003, Saudia ilianzisha tena uhusiano na Iraq kwa ngazi ya uwakilishi na mwaka huo huo uhusiano huo ulipandishwa juu zaidi hadi kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia. Mwezi Disemba mwaka 2015 kulifunguliwa ubalozi wa Saudia mjini Baghdad. Hata hivyo mienendo ya chuki na uingiliaji wa ubalozi wa Saudia katika masuala ya ndani ya Iraq, na kadhalika uungaji mkono wa wazi na wa siri wa ubalozi huo kwa makundi ya kigaidi nchini Iraq vilipelekea kusambaratika fursa za kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande hizo mbili. Baada ya kuzorota uhusiano baina ya Iraq na Saudia na katika kuendeleza siasa zake za uhasama dhidi ya Iraq, Riyadh ilipunguza kiwango cha uhusiano wake wa kidiplomasia na kufikia ngazi ya ubalozi mdogo.
Kwa sasa na baada ya kutathmini hali ya mambo nchini Iraq utawala wa Aal-Saud umechukua hatua ya ghafla ya kumtangaza balozi wake mdogo nchini Iraq. Katika miaka ya hivi karibuni, siasa za kigeni za Saudia, zimebiniwa kwa msingi wa kuwaunga mkono wapinzani wa serikali kuu ya Iraq, kuchochea serikali ya eneo la Kurdistan dhidi ya serikali kuu ya Baghdad, na kuzishawishi koo za Waislamu wa Kisuni kwa ajili ya kuanzisha upinzani dhidi ya serikali kuu ya nchi hiyo.
Mienendo hiyo ndio sababu ya taifa la Iraq kuitaka serikali ya nchi hiyo kuangalia upya mwenendo wake na Riyadh sambamba na kuchukua hatua za dhati za kukabiliana na uingiliaji wa kihasama wa Aal-Saud nchini humo.
Ni kwa kuzingatia siasa za uingiliaji na za uhasama za utawala wa Saudia ndio maana watu wa Iraq wakawa na mitazamo hasi na ya dhana mbaya kuhusiana na mienendo ya Saudia na kuzifuatilia kwa makini sana harakati zote za kisiasa za utawala wa Saudi Arabia nchini mwao zikiwemo safari za kimaonyesho tu viongozi wa utawala huo mjini Baghdad.
Hali ya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati inaonyesha kwamba, utawala wa Aal-Saud unachukiwa sana katika eneo hilo na kimataifa kutokana na uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi kama Daesh na uingiliaji wake katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.