Nguruwe mwitu wenye hasira waua magaidi wa ISIS nchini Iraq
Magaidi watatu wa kundi la kitakifiri la ISIS au Daesh wameuawa na nguruwe mwitu waliokuwa na hasira katika eneo la kaskazini mwa Iraq.
Kwa mujibu wa jarida la Iraq News, magaidi hao watatu wa ISIS waliuawa na nguruwe mwitu hao katika eneo la kusini mwa Kirkuk. Taarifa zinasema magaidi wengine watano walijeruhiwa vibaya na nguruwe mwitu hao. Mkuu wa kabila la Ubaid katika eneo hilo Sheikh Anwar al-Assi amesema kabla ya kushambuliwa na nguruwe mwitu, magadi hao walikuwa wakipanga kutekeleza hujuma ya kuvizia dhidi ya wakaazi wa eneo hilo ambao wameunda brigedi za kukabiliana na kundi la kigaidi la ISIS.
Sheikh al-Assi ameongeza kuwa, magaidi sugu wanane walikuwa wamejificha katika msitu karibu na mto ujulikanao kama Zaghitoun wakati waliposhambuliwa na nguruwe mwitu hao waliokuwa na hasira. Imearifiwa kuwa baada ya tukio hilo, magaidi waliosalia walichukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya wanyama hao lakini haijabainika ni mbinu ipi waliyotumia.
Kabla ya magaidi hao kuuawa na nguruwe mwitu, walikuwa wamewaua wakaazi 25 wa eneo hilo katika kipindi cha siku tatu. Mauaji hayo yalitekelezwa katika eneo la Hawija yapata kilomita 100 kutoka mji wa Mosul. Kwa muda wa miezi sita sasa wanajeshi wa Iraq wamekuwa wakitekeleza oparesheni maalumu za kuukomboa kikamilifu mji wa Mosul kutoka mikononi mwa ISIS.