Wanajeshi wa Saudia waendeleza hujuma katika mji wa Al Awamiyah
Baada ya kupita wiki mbili tokea wanajeshi wa Saudi Arabia wavamie mtaa wa Al Masourah mjini Al-Awamiya mashariki mwa nchi hiyo hali inaripotiwa kuwa mbaya huku ukandamizaji ukiendelea.
Wanajeshi wa Saudia wameteketeza moto misikiti, nyumba za raia na shule katika mtaa huo huku jamii ya kimataifa ikiwa inaendelea kunyamazia kimya jinai hiyo.
Siku ya Jumatano wanajeshi wa Saudia waliendeleza hujuma mashariki mwa Saudia kwa kudondosha mabomu katika eneo hilo.
Watawala wa Saudia wanataka kukiharibu kijiji cha al-Masourah ambako ndiko alikozaliwa Sheikh Nimri Baqir an-Nimr, mwanazuoni mkubwa wa Waislamu wa Kishia aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na utawala huo mwaka jana. Watawala hao wa Saudia wamekivamia kijiji hicho kwa madai ya eti kukiboresha.
Kijiji cha al-Masourah kinafahamika kama nembo ya malalamiko huko mashariki mwa Saudia dhidi ya watawala wa nchi hiyo ya kidikteta.