Maadhimisho ya siku ya ukombozi wa kusini mwa Lebanon
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, kuna udharura wa kubakishwa hai na kurithishwa vizazi vijavyo mafanikio ya muqawama wa wananchi wa Lebanon katika mapambano yao na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wakati huo huo viongozi mbalimbali wa kijeshi na kiusalama wa Lebanon nao wamesisititizia udharura wa kusimama imara kukabiliana na njama zote za Wazayuni na magenge ya wakufurishaji. Mwito huo umetolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kukombolewa kusini mwa Lebanon kutoka katika makucha ya Wazayuni.
Brigedia Jenerali Joseph Oun, mkuu wa jeshi la Lebanon ametoa tamko kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 17 wa kukombolewa kusini mwa Lebanon kutoka katika makucha ya utawala wa Kizayuni na kuvitaka vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kuzidi kujiimarisha kwa ajili ya kuilinda ardhi, wananchi na maliasili za Lebanon.
Tarehe 25 Mei 2000, ni siku ya ushindi wa muqawama wa Kiislamu wa Lebanon dhidi ya utawala wa Kizayuni ambao ulilikalia kwa mabavu eneo la kusini mwa Lebanon kwa muda wa miaka 22.
Katika taarifa yake hiyo maalumu, kamanda wa jeshi la Lebnaon amesema, macho ya Walebanon yameelekezwa kwa watu ambao wamesimama imara kulinda mipaka ya nchi hiyo mbele ya adui Mzayuni na magenge ya kigaidi.
Tarehe 25 Mei 2000 ilikuwa ni siku muhimu mno katika historia ya mapambano dhidi ya Wazayuni katika eneo zima la magharibi mwa Asia. Hatimae baada ya mapambano ya maiaka 22, wanamapambano wa Kiislamu wa Lebanon walivuna matunda ya mapambano yao baada ya kutoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuulazimisha kukimbia kwa fedheha kutoka kusini mwa Lebanon. Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza rasmi kupata utawala wa Kizayuni wa Israel mbele ya muqawama wa wananchi wa Lebanon na kiujumla kulikuwa ni kushindwa vibaya na kuaibika utawala huo dhalimu tangu ulipopandikizwa na madola ya Magharibi katikati kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu. Hadi wakati huo, utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa unajilabu na kujigamba kuwa haushindiki.
Tangu madola ya kikoloni yalipoupandikiza utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili nyeti mwaka 1948, walimwengu wameshuhudia vita vingi baina ya utawala huo ghasibu na nchi za Mashariki ya Kati ikiwemo Lebanon. Haikuwahi kutokezea hata mara moja nchi za Kiarabu kuushinda utawala wa Kizayuni wa Israel. Mwaka 1982 na baada ya kupata jeuri kubwa zaidi, utawala wa Kizayuni ulifananya mashambulizi makubwa nchini Lebanon na kuliteka eneo la kusini mwa nchi hiyo. Lengo la Israel lilikuwa ni kuiteka kikamilifu ardhi ya Lebanon, lakini wananchi wa nchi hiyo wasingeliweza kabisa kuvumilia uvamizi huo. Lengo la Israel tangu kupandikizwa kwake kwenye eneo hili, lilikuwa ni kuunda dola kubwa la Mayahudi linaloanzia Mto Nile Misri hadi Mto Furat. Hata hivyo wananchi Waislamu wa Lebanon wamekuwa mwiba mchungu uliosambaratisha ndoto hiyo ya Wazayuni. Wananchi hao walianzisha muqawama wa Kiislamu ukiongozwa na Hizbullah na kuvuruga ndoto zote za utawala wa Kizayuni. Matokeo ya mapambano hayo ni kulazimika wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kukimbia kwa fedheha kusini mwa Lebanon mwaka 2000. Kushindwa huko kulikuwa mwanzo wa mlolongo wa kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vyake na muqawama wa Lebanon. Mwaka 2006, Israel ilianzisha vita vingine vya siku 33 dhidi ya Lebanon kwa lengo la kuisambaratisha kabisa Hizbullah, lakini pigo ulilopata utawala wa Kizayuni katika vita hivyo ni kubwa mno kiasi kwamba Wazayuni walilazimika kuwaachilia huru mateka wengi wa Palestina na Lebanon ikiwa ni kutii matakwa ya Hizbullah kwa ajili ya kurejeshewa miili ya wanajeshi wawili wa Israel waliouliwa na Hizbullah.
Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba muqawama wa wananchi wa Lebanon unaoongozwa na Hizbullah umekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi hiyo na kuleta athari kubwa pia kieneo na kimataifa. Ushindi mbalimbali inaopata muqawama dhidi ya Wazayuni umeitangaza na kuiletea sifa nzuri Lebanon na wananchi wake na kuvunja njama za maaadui; maadui ambao wanafanya njama mbalimbali za kutoa pigo kwa nchi hiyo na kila taifa linalopambana na Israel. Miongoni mwa njama za mabeberu ni kuanzishwa magenge ya kitakfiri na kuyatuma katika nchi kama Syria na Lebanon ili kufidia kushindwa vibaya Israel na harakati ya muqawama. Hata kipigo kikali na kufedheheshwa Israel cha tarehe 25 Mei 2000 ni jambo ambalo linapuuzwa kikamilifu na vyombo vya habari vya Magharibi na vibaraka wao, yote hayo ni katika kujaribu kuficha kushindwa vibaya Israel. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndipo tutaweza kuelewa ni kwa nini Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah akatilia mkazo suala la kubakishwa hai matukio hayo na kurithishwa vizazi vijavyo ushindi mkubwa inaoendelea kupata muqawama katika mapambano yake na utawala wa Kizayuni wa Israel.