Saudia yatabiri kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Qatar
Katika hali inayoonekana ni ya kuzidi kuvurugika uhusiano wa Saudi Arabia na Qatar, gazeti moja la Saudia linalochapishwa mjini Riyadh limetabiri kuwa, kuna uwezekano wa kutokea mapinduzi ya sita ya kijeshi nchini Qatar hasa kwa kuzingatia katika nchi hiyo ndogo ya Kiarabu kumetokea mapinduzi matano ya kijeshi katika kipindi cha baina ya mwaka 1971 na 2013.
Jana Ijumaa, shirika la habari la IRNA lililinukuu gazeti la al Riyadh la Saudi Arabia likiandika kuwa, licha ya kupita miaka minne ya utawala wa Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani lakini hadi hivi sasa mfalme huyo kijana ameshindwa kupata rafiki angalau mmoja, na kinyume chake ni kuwa amepata maadui wengi.
Gazeti hilo la Saudi Arabia limeongeza kuwa, tishio la kwanza kabisa linalomkabili mfalme wa Qatar ni kutoka kwa watu wa familia ya Ahmad bin Ali kwani wao ndio wenye haki ya kisheria ya kutawala Qatar, hivyo watakuwa na hamu ya kulipiza kisasi kutoka kwa amiri wa hivi sasa wa nchi hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, yote hayo ni matokeo mabaya ya ziara ya hivi karibuni ya rais wa Marekani, Donald Trump nchini Saudi Arabia. Katika ziara yake hiyo ya mwisho mwa mwezi uliopita wa Mei, Trump alitiliana saini na Saudi Arabia mkataba wa silaha wa mabilioni ya dola za Kimarekani za kuulinda utawala wa Aal Saud.
Qatar ilishiriki katika mkutano wa Riyadh uliowakutanisha baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu na rais wa Marekani, Donald Trump. Mzozo na hitilafu kubwa baina ya Qatar na Saudi Arabia zilionekana waziwazi kwenye mkutano huo wa Riyadh.