Wapiganaji wa Ansarullah wamuangamiza afisa wa jeshi la Saudia
Wapiganaji wa Harakati ya Ansarullah nchini Yemen wamepambana vikali na wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia katika maeneo ya mipakani na kumuangamiza afisa wa jeshi la Saudia mwenye cheo cha kapteni.
Shirika rasmi la habari Saudia SPA limekiri Jumamosi kuwa Kapteni Mohammad bin Eid bin Abdullah al Subaei wa kikosi cha nchi kavu cha jeshi la ufalme huo aliuawa siku kadhaa zilizopita wakati wapiganaji wa Ansarullah walipotekeleza hujuma dhidi ya kituo kimoja cha ulinzi mpakani kusini mwa Saudia.
Wanajeshi wa Yemen wakishirikiana na wapiganaji wa Ansarullah mara kwa mara hutekeleza oparesheni kubwa ya kulipiza kisasi dhidi ya askari vamizi wa Saudi Arabia na waitifaki wao ambao wamekuwa wakitekeleza hujuma za kila siku dhidi ya nchi hiyo tokea Machi 2015.
Saudia iliivamia Yemen kwa uungaji mkono wa Marekani kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Raia zaidi ya elfu 13 wa Yemen wameuawa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukishindwa kuchukua hatua yoyote ya kuzuia jinai hizo za Saudia huko Yemen.