Qatar yaafiki upatanishi wa Kuwait katika mgogoro na Saudia
(last modified Tue, 06 Jun 2017 13:40:26 GMT )
Jun 06, 2017 13:40 UTC
  • Qatar yaafiki upatanishi wa Kuwait katika mgogoro na Saudia

Qatar imesema iko tayari kuipa Kuwait fursa kuwa mpatanishi katika mgogoro ulioibuka baada ya Saudi Arabia kuzichochea nchi kadhaa za Kiarabu kukata uhusiano na nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammad bin Abdulrahman al-Thani amesema leo kuwa, Amir wa Qatar ametangaza kuwa tayari kwa ajili ya upatanishi wakati alipofanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Kuwait.

Siku ya Jumatatu Saudia iliongoza Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Misri, Libya, Maldives na Mauritius katika kukata uhusiano na Qatar. Aidha nchi hizo zimekata uhusiano wa anga, bahari na nchi kavu na Qatar. Saudia imechukua hatua hiyo kwa madai kuwa Qatar inaunga mkono makundi ya kigaidi na inaingilia mambo ya ndani ya nchi zingine za Kiarabu.

Mohammad Javad Zarif

Wakati huo huo Iran pia iko mbioni katika kufanya mazungumzo na nchi kadhaa ili kusuluhisha mgogoro ulioibuka. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amefanya mazungmo na mwenzake wa Qatar. Aidha Zarif amezungumza kwa njia ya simu na mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Oman, Kuwait, Indonesia, Iraq, Tunisia, Malaysia, Lebanon na Algeria pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ili kujadili kadhia hiyo ya mgogoro wa Qatar na baadhi ya nchi jirani.

Duru zinasema Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yusuf bin Alawi bin Abdullah amesafiri leo Kuwait kujadili njia za kupunguza mgogoro ulioibuka huku  afisa wa ngazi za juu wa Saudia naye akiripotiwa kutembelea Kuwait kujadili kadhia hiyo.

 

Tags