Mauritania nayo yakata uhusiano na Qatar, Gabon yaishutumu Doha
(last modified Wed, 07 Jun 2017 07:09:23 GMT )
Jun 07, 2017 07:09 UTC
  • Mauritania nayo yakata uhusiano na Qatar, Gabon yaishutumu Doha

Katika hatua inayoonekana ni kufuata kibubusa sera za Saudi Arabia, Mauritania imetangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar, siku chache baada ya nchi kadhaa za Kiarabu kuchukua hatua kama hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika imesema taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limeamua kukata uhusiano wake na Qatar eti kwa kuwa inaunga mkono magenge ya kigaidi na kuenea kwa misimamo mikali ya kufurutu ada duniani.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kitendo hicho cha Qatar kuunga mkono harakati za ugaidi duniani kimepelekea kuteketezwa roho za watu wasio na hatia hususan katika nchi za Kiarabu na bara Ulaya.

Bendera za baadhi ya nchi zilizochochewa na Saudia kukata uhusiano na Qatar

Wakati huo huo, Gabon, nchi ya katikati mwa Afrika yenye utajiri mkubwa wa mafuta kwa upande wake licha ya kutotangaza kukata uhusiano na Qatar, imeikashifu na kuikosoa vikali Qatar, eti kwa kukataa kufuata na kuheshimu jitihada za kimataifa za kupambana na ugaidi.

Siku ya Jumatatu utawala wa Saudia uliongoza Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Misri, Libya, Maldives na Mauritius katika kukata uhusiano na Qatar. Aidha nchi hizo zimekata uhusiano wa anga, bahari na nchi kavu na Qatar.

Hii ni katika hali ambayo, Qatar kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imesisitiza kuwa, hatua hiyo ya kukata uhusiano nayo imechukuliwa kwa kutegemea madai ya urongo na yasiyo na msingi.

 

Tags