Russia: Kuna uwezekano mkubwa kiongozi wa Daesh ameuawa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi ameangamizwa.
Oleg Syromolotov amesema, kuna uwezekano mkubwa kwamba Abu Bakr al Baghdadi aliuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Russia nchini Syria.
Syromolotov ameongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa za kipelelezi za Wizara ya Ulinzi ya Russia, ni kwamba al Baghdadi aliuawa katika shambulizi lililolenga ofisi za uongozi wa kundi la Daesh katika viunga vya mji wa Raqqah mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Moscow inafanyia uchunguzi zaidi taarifa hizo.
Amesema kuwa mauaji ya kiongozi wa Daesh yatapelekea kusambaratika uongozi wa kundi hilo na kuzusha woga na hofu katika safu za wapiganaji wake.
Siku chache zilizopita pia Wizara ya Ulinzi ya Rusia ilitangaza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba, kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi ameuawa na kwamba inafanya jitihada za kuchunguza kwa undani zaidi habari hiyo.
Ripoti hiyo ilisisitiza kuwa, maafisa 34 wa ngazi za juu wa kundi la Daesh na makamanda 300 wa kundi hilo waliuawa katika shambulizi hilo.