Rais Rouhani: Iran imeazimia kupanua zaidi mahusiano na Qatar
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Aal Thani ambapo sambamba na kumuhakikishia kuwa, serikali na taifa la Iran liko pamoja na serikali na taifa la Qatar, amesema kuwa, siasa za Tehran zimelenga kuimarisha mahusiano zaidi na Doha.
Rais Hassan Rouhani alisema hayo Jumapili ya jana alipompigia simu amir huyo wa Qatar ambapo sambamba kumpa salamu za Iddil-Fitri na kusema kuwa, kuisaidia Qatar kuimarisha uchumi wake hasa katika kipindi hiki kigumu na kustawisha uhusiano wa pande mbili hususan katika sekta maalumu, ni malengo ya pamoja baina ya Jamhuri ya Kiislamu na serikali ya Doha.
Amesema kuwa, Tehran inaamini kuwa, mashinikizo, vikwazo au vitisho vinavyofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu dhidi ya Qatar, haviwezi kutatua tofauti zilizopo kati ya nchi za eneo hili. Akiashiria uhusiano uliopo kati ya Iran na Qatar kwa ajili ya maslahi ya raia wa nchi hizo, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, mtazamo wa Tehran juu ya ushirikiano na serikali ya Doha, ni mtazamo endelevu wa kuimarisha na kuboresha zaidi mahusiano ya pande mbili. Pia amemuhakikishia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari kufanya juhudi zake zote kuhakikisha kuwa matatizo yaliyopo yanatatuliwa kwa njia za amani, ili kuliletea eneo la Mashariki ya Kati amani na utulivu.
Kwa upande wake Amir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani sambamba na kushukuru na kupongeza uungaji mkono wa serikali na taifa la Iran kwa serikali na taifa lake, amesema kuwa, mahusiano ya Iran na Qatar ni yaliyofungamana juu ya msingi wa ustawishaji wa mahusiano na kwamba sambamba na Doha kuwa tayari kupanua wigo wa mahusiano hayo ya pande mbili, ipo tayari pia kushirikiana na Iran ya Kiislamu kwa ajili ya kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo, kabla ya hapo Mkuu wa Vyombo vya Mahkama nchini Iran, Ayatullah Amoli Larijani alikuwa amekosoa vikali mzingiro wa anga, baharini na nchi kavu dhidi ya Qatar, na kusema kuwa, Tehran itafungua mipaka yake yote kwa ajili ya nchi jirani ya Qatar.