Kundi la pili la wanajeshi wa Uturuki limewasili Qatar
(last modified Fri, 30 Jun 2017 08:11:55 GMT )
Jun 30, 2017 08:11 UTC
  • Kundi la pili la wanajeshi wa Uturuki limewasili Qatar

Televisheni rasmi ya Qatar leo asubuhi imetangaza kuwa, kundi jipya la wanajeshi wa Uturuki limewasili katika kambi ya jeshi la anga ya al Adida iliyopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Doha.

Waziri wa Ulinzi wa Qatar amesema kuwa, kundi la pili la wanajeshi wa Uturuki limewasili katika kituo hicho cha anga cha al Adida ili kuungana na wenzao waliopo Doha. Kundi la kwanza la wanajeshi wa Uturuki liliwasili nchini Qatar siku kadhaa zilizopita. 

Uturuki inatuma wanajeshi huko Qatar katika hali ambayo nchi nne yaani Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misrizimetaka kufungwa kwa kituo cha kijeshi cha Uturuki huko Doha kama sharti la kuanzisha tena uhusiano na Qatar. 

Wanajeshi wa Uturuki baada ya kuwasili Doha, Qatar   

Saudia, Misri, Imarati na Bahrain ambazo tangu tarehe 5 mwezi huu zilikata mahusiano yao ya kidiplomasia na Qatar zikiituhumu nchi hiyo kuwa inayaunga mkono makundi ya kigaidi, zimeikabidhi Doha orodha ya matakwa yao yenye vipengee 13. Nchi hizo nne zimesema kuwa kuhuishwa uhusiano kati yao na Doha kutategemea utekelezwaji wa matakwa hayo yote.

Akitoa jibu kwa matakwa hayo, Muhammad bin Abdulrahman Aal Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema kuwa: Doha iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu masuala halali yanazowahusu majirani zake katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo amesisitiza kuwa, baadhi ya matakwa hayo kamwe hayawezi kutekelezwa kutokana na kuwa si ya kimantiki na kwamba Qatar haiwezi kusalimu amri mkabala na haki yake ya kujitawala. 

Tags