Utunishaji misuli dhidi ya Qatar na masharti yasiyotekelezeka ya Saudia
Saudi Arabia na waitifaki wake wamezidi kuitunishia misuli Qatar kwa kuipa masharti 13 magumu ambayo ni muhali kutekelezeka. Viongozi wa nchi mbalimbali, wanasiasa mashuhuri wa kieneo na kimataifa akiwemo pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, wote wamesema kuwa masharti hayo hayatekelezeki.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Muhammad bin Abdulrahman Aal Thani amesema kuwa, nchi yake ilipokea orodha ya masharti hayo 13 wiki iliyopita na ndani yake mna mambo ambayo ni muhali kutekelezeka.
Mgogoro baina ya Qatar na Saudia na waitifaki wake ulizuka Jumatatu tarehe 5 Juni. Mapema siku hiyo, ghafla moja, Saudi Arabia ilizuka na kutangaza kukata uhusiano wake wa pande zote na Qatar na muda mchache baadaye nchi za Bahrain, Imarati na Misri nazo zikatangaza msimamo huo huo. Katika kuhalalisha hatua yao hiyo ya kushitukiza, nchi hizo nne zilidai kuwa Qatar inahatarisha usalama wao, inaingilia masuala yao ya ndani na inaunga mkono ugaidi.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, masharti yaliyotolewa na Riyadh na waitifaki wake yanalenga moja kwa moja kwenye hadhi na utambulisho. Kwa upande wa Qatar, kutekeleza masharti hayo kuna maana ya kupoteza utambulisho wake. Miongoni mwa mashrti hayo ni kuitaka Qatar ikate uhusiano wake na jirani yake muhimu yaani Iran na hapo Saudia na wenzake wanaonekana kuhusisha uhusiano wa Usuni katika mkabala wa Ushia. Vile vile zimeitaka Qatar ifunge kambi ya kijeshi ya Uturuki mjini Doha, na hapo nchi hizo zinaonekana kulenga utambulisho wa Ikhwanul Muslimin katika mkabala wa Uwahabi. Pia wameitaka Doha ifunge kituo chake cha televisheni cha al Jazeera, na hapo inaonekana wazi zimelenga kwenye utambulisho wa vyombo vya habari vinavyozikosoa tawala za nchi za Kiarabu. Hata hivyo masharti hayo si tu yamekataliwa na viongozi wa Qatar, lakini wachambuzi wa mambo nao wamesema hayaingii akilini hata kidogo. Dk Max Abrahms ni mchambuzi maarufu wa masuala ya kimataifa amesema kuhusu masharti hayo ya Saudia na waitifaki wake kwa Qatar kwamba: Iwapo Qatar itakubali kutekeleza masharti hayo, basi hakutakuwa tena na nchi inayoitwa Qatar kwani yamelenga moja kwa moja kwenye uhuru wa kisiasa wa Qatar na nafasi yake katika eneo hili.
Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni nini lengo la Saudia la kutoa masharti hayo yasiyotekelezeka? Inavyoonekana ni kwamba viongozi wa Riyadh waliotwaa madaraa ya nchi hiyo tangu mwezi Januari 2015 hususan Mohammed bin Salman, mrithi mpya wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, wana uchu wa kuzusha migogoro katika eneo la Asia Magharibi ili kutumisha misuli ndani ya Saudia na nje ya nchi hiyo ya kifalme. Bin Salman anatambua vyema kuwa, wananchi wa Saudi Arabia wanalipa umuhimu mkubwa suala la nchi yao kuwa na nafasi muhimu katika eneo hili. Hata hivyo njia zinazotumiwa na bin Salman za kutaka Saudia iwe na nafasi muhimu katika eneo hili ni ghalati. Riyadh imeanzisha vita vya kivamizi dhidi ya nchi maskaini zaidi ya Kiarabu katika eneo la Mashariki ya Kati yaani Yemen na kabla hali haijatulia amejitia kwenye mgogoro na Qatar. Kabla ya hapo Saudia ilianza kuunga mkono waziwazi magenge ya kigaidi yanayofanya jinai katika nchi kama za Iraq na Syria. Sasa yote hayo si tu hayaifanyi nafasi ya Saudi Arabia kuonekana nzuri katika eneo hili, bali yanazidi kuporomosha heshima ya nchi hiyo kieneo na kimataifa hususan kutokana na kueneza kwake fitna za kimadhehebu na kikabila tena na kufeli katika nchi zote ambazo Saudia imejiingiza kwenye migogoro nazo.
Kwa kweli matunda ya migogoro iliyoanzishwa na viongozi wapya wa Saudia kwa nia ya kuonesha Riyadh ina nguvu si jambo jingine isipokuwa kuzidi kuonekana uanagenzi na kutokuwa na mtazamo wa mbali viongozi wa nchi hiyo. Madhara mengine ya siasa hizo za Saudi Arabia ni kudhoofika nafasi yake katika eneo hili na vile vile kuteteresha vibaya misingi ya utawala wa nchi hiyo. Inaonekana wazi kwamba, masharti magumu yaliyotolewa na Saudi Arabia kwa Qatar hayana lengo jengine isipokuwa kutaka kuidhibiti nchi hiyo kama anavyosema Abdul Bari Atwan, mchambuzi maarufu wa masuala ya ulimwengu wa Kiarabu ambaye amesema: "Inaonekana wazi kwamba masharti iliyowekewa Qatar ni masharti yaliyowekwa kwa makusudi ili yasitekelezeke na hivyo kuilazimisha Doha iyakatae ili kuzipa fursa nchi zilizoweka masharti hayo zichukue hatua kali zaidi dhidi ya Qatar."