Uanachama rasmi wa Palestina katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA)
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3160-uanachama_rasmi_wa_palestina_katika_mahakama_ya_kudumu_ya_usuluhishi_(pca)
Palestina imekuwa mwanachama rasmi wa Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 16, 2016 03:23 UTC
  • Uanachama rasmi wa Palestina katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA)

Palestina imekuwa mwanachama rasmi wa Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi.

Palestina imekubaliwa kuwa mwanachama rasmi wa mahakama hiyo kwa kupigiwa kura 57 za 'ndiyo' huku wanachama 24 wakiamua kutopiga kura. Hakuna nchi mwanachama iliyopiga kura ya 'hapana'.

Palestina iliwasilisha ombi la uanachama kwa serikali ya Uholanzi ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuchunguza maombi ya uanachama na ikatangazwa rasmi kuwa mwanachama wa PCA tarehe 29 Januari mwaka uliopita wa 2015. Hata hivyo Marekani, utawala haramu wa Israel na Canada zililalamikia uanachama wa Palestina na kumfanya Mkuu wa Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi asimamishe kwa muda uanachama huo na kuamuliwa suala hilo lijadiliwe na kuamuliwa na kamati maalumu ya mahakama hiyo.

Riyadh al-Maliki, mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa alitaka shauri la kusimamishwa uanachama wa Palestina liangaliwe upya. Na hivi sasa baada ya kupita mwaka mmoja wa kuchelewesha uchunguzi wa suala hilo sambamba na vikao mbalimbali vya kidiplomasia vilivyofanyika baina ya ujumbe wa Palestina na maafisa wa nchi mbalimbali huko Uholanzi, vilivyoambatana na uungaji mkono wa wanachama wa Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi, hatimaye Palestina imepata uanachama wa kudumu wa mahakama hiyo bila ya kupingwa na mwanachama yeyote.

Baada ya ujumbe wa Marekani kubaini kuwa hauwezi kuendeleza uafriti wa kukwamisha uanachama wa Palestina katika PCA ulilazimika kutoka nje ya ukumbi wa kupigia kura kama ishara ya kuonyesha malalamiko.

Ombi la uanachama wa Palestina katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi liliwasilishwa kwenye taasisi hiyo baada ya Marekani kuupigia kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mpango wa kutaka kukomeshwa ukaliwaji wa mabavu wa ardhi za Palestina. Kwa kupata uanachama wa PCA, Wapalestina wataweza kuomba kuchunguzwa jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa, na vilevile kuhusu ujenzi wa vitongoji wa walowezi wa Kiyahudi katika ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Utawala wa Kizayuni umeweka rekodi ya kuandamwa na taarifa na maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa kutokana kuivamia na kuikalia kwa mabavu Palestina na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanya katika ardhi hizo. Kutolewa zaidi ya maazimio mia moja katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama pamoja na taasisi nyengine za umoja huo hususan Baraza la Haki za Binadamu dhidi ya Israel ni ithbati na ushahidi wa wazi wa dhulma ambazo wamekuwa wakifanyiwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Umoja wa Mataifa umetoa wito mara kadhaa wa kutaka kuundwa nchi huru ya Palestina, lakini Israel imekwamisha suala hilo kutokana na uungaji mkono inaopata kwa Marekani. Na kwa kuzivamia na kuzikalia kwa mabavu ardhi nyengine za Palestina wakati wa vita vya mwaka 1967, imefunga njia zote za kuwezesha kuundwa nchi hiyo.

Katika hali kama hiyo, na baada ya kuvunjika mazungmzo ya mapatano ya Mashariki baina utawala wa Kizayuni na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, ambayo yamekuwa yakifanyika kwa upatanishi wa Marekani; na vilevile kutokana na kupinga Washington kupitishwa maazimio dhidi ya Israel katika Baraza la Usalama, ndipo Wapalestina wakaamua kuingia kwenye uga wa sheria za kimataifa ili kupigania kurejeshewa haki zao zilizoporwa kwa miaka inayokaribia 70 sasa.

Kuwasilishwa suala la jinai za kivita zilizofanywa na Israel katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi kutawagharimu mno Wazayuni; na nchi kadhaa zinazoendesha kampeni ya kuususia utawala haramu wa Kizayuni zitasimama dhidi ya utawala huo ghasibu.../