Qatar yaionya Saudia na hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Doha
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar ameionya Saudi Arabia kuhusiana na kuchukua hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi yake.
Mohammed bin Abdulrahman Al Thani ameihutubu Saudia na kutangaza kuwa, chaguo la kijeshi litakuwa na matokeo mabaya na litaligharimu pakubwa eneo la Mashariki ya kati.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amesisitiza kuwa, nchi yake haitasalimu amri mbele ya matakwa yasiyo ya kisheria ya nchi zilizoiwekea vikwazo nchi hiyo zikiongozwa na Saudi Arabia.
Mohammed bin Abdulrahman Al Thani ameeeleza kuwa, hakuna mgogoro ambao unaweza kutatuliwa kupitia njia ya makabiliano ya moja kwa moja, bali mivutano siku zote hupatiwa ufumbuzi kupitia njia ya mazungumzo.
Amesema kuwa, utawala wa Saudia unapaswa kufahamu kwamba, kushadidisha hatua dhidi ya Qatar na kutekeleza chaguo la kijeshi dhidi ya nchi yake ni hatua ambayo italigharimu pakubwa eneo la Mashariki ya Kati. Amesisitiza kuwa, Qatar katu haikubaliani na matakwa ambayo ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.
Nchi nne yaani Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zimeiwekea vikwazo Qatar tangu tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu. Nchi hizo nne za Kiarabu tarehe 23 mwezi Juni mwaka huu ziliipatia Qatar masharti yenye vipengee 13 ili kurejesha uhusiano wao na nchi hiyo, matakwa ambayo hata hivyo yemepingwa na Doha ikisema kuwa hayana mlingano, si ya kimantiki na hayawezi kutekelezeka.