Wapalestina wengine wawili wauawa shahidi na jeshi la Israel
Jeshi katili la utawala wa kizayuni wa Israel limeua shahidi vijana wawili wa Kipalestina, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Mashuhuda wanasema kuwa, askari hao wa utawala haramu wa Israel wamewamiminia risasi vijana hao katika kitongoji cha Ariel mjini Salfit, eti kwa madai ya kuhusika katika wimbi la kuwadunga kisu wanajeshi wa utawala huo katili. Wawili hao wameuawa wakishiriki maandamano ya kulaani hujuma na jinai za kutisha zinazofanywa na jeshi la wazayuni dhidi ya Wapalestina, ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu. Wapalestina zaidi 200 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.
Wakati huo huo, askari mmoja na mlowezi wa kizayuni wametishia kumuua mwandishi wa habari wa Kipalestina Muhammad al-Qiq, ambaye alisusia chakula kwa takriban siku mia moja. Wawili hao wanadaiwa kuingia kwa nguvu katika hospitali ya al-Afula na kumfokea kijana huyo wa Kipalestina kwa kumwabia: “Lazima ufe, wewe hufai chochote ila kufa.” Mke wa mwanahabari huyo Fayhaa Shalash amesema kuwa wazayuni hao wawili wenye misimamo mikali walitoroka hospitalini hapo baada ya al-Qiq kupige makelele ya kuomba msaada. Al-Qiq ambaye alikataa kula kwa siku 94 kulalamikia hatua ya jeshi la kizayuni kumzuilia kinyume cha sheria, alisitisha mgomo wa kula Februari 26 na sasa anaendelea kutibiwa katika mji wa Ramallah, huko Ukingo wa Magharibi.