Hizbullah: Lebanon sio nchi tena inayoogopa kupambana na utawala wa Israel
Mjumbe wa Baraza Kuu la harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Nabil Qaouk amesema kuwa Lebanon sio taifa ambalo linaogopa kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel au magenge ya ukufurishaji.
Sheikh Nabil Qaouk ameyasema hayo kwa mnasaba wa sherehe za mwaka wa 11 wa ushindi wa harakati ya ya Hizbullah katika vita vya siku 33 mwaka 2006 na utawala ghasibu wa Kizayuni eneo la Sidon na kuongeza kuwa, ushirikiano wa jeshi la serikali ya Lebanon na harakati ya Hizbullah unaweza kuyakomboa maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni na makundi ya kigaidi.
Sherehe hizo za mwaka wa 11 wa ushindi wa harakati ya Hizbullah katika vita vya siku 33 mwaka 2006, zilihudhuriwa na wanasiasa, jumbe za vyama vya kisiasa, makundi ya Palestina, wasomi wa kidini na wageni wengine waalikwa.
Vita vya siku 33 kati ya wapiganaji shupavu wa Hizbullah na utawala ghasibu wa Israel vilianza Julai mwaka 2006 na kufikia tamati tarehe 14 Agosti. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulipata kipigo na hasara kubwa na kulazimika kusitisha mashambulizi.
Katika fremu hiyo hiyo, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya nchini Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, kushindwa na kufedheheka vitaandamana na utawala haramu wa Israel katika vita yoyote ile itakayotokea.