Marekani yaendeleza ukatili, yaua raia 38 katika hujuma za anga Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33248-marekani_yaendeleza_ukatili_yaua_raia_38_katika_hujuma_za_anga_syria
Ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani zimeendeleza hujuma zake za kikatili, na mara hii zimeua raia 38 katika mji wa Raqqah kaskazini mwa Syria, ndani ya masaa 48 yaliyopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 17, 2017 06:48 UTC
  • Marekani yaendeleza ukatili, yaua raia 38 katika hujuma za anga Syria

Ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani zimeendeleza hujuma zake za kikatili, na mara hii zimeua raia 38 katika mji wa Raqqah kaskazini mwa Syria, ndani ya masaa 48 yaliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la Syrian Observatory for Human Rights (SOHR) lenye makao makuu yake mjini London, wanawake 2 na watoto 5 ni miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulizi ya ndege za kivita za muungano wa kijeshi eti wa kupambana na ugaidi unaoongozwa na Marekani nchini Syria.

Aidha shirika hilo limesema watu wengine 30 wamejeruhiwa katika hujuma hizo za jana Jumatano, katikati ya mji wa Raqqah, mbali na kuharibiwa miundombinu. 

Mauji hayo ya raia yanajiri chini ya siku 10, baada ya ndege hizo za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na US kushambulia makazi ya watu katika mji huo huo wa Raqqah na kuua watu 30. 

Ndege za kivita za Marekani zinazoua raia Syria

Ndege hizo mara kwa mara zimekuwa zikiwaua raia wa Syria wasio na hatia wala ulinzi kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi. 

Mapema mwezi huu, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika kile kinachoitwa vita vya kupambana na ugaidi ulitangaza katika takwimu zake za kila mwezi kuwa umeua raia 624 kwenye mashambulizi ya anga uliyofanya katika nchi za Iraq na Syria.