UN: Hujuma za Saudi zimesababisha nusu ya vifo vya watoto Yemen
(last modified Fri, 18 Aug 2017 08:08:53 GMT )
Aug 18, 2017 08:08 UTC
  • UN: Hujuma za Saudi zimesababisha nusu ya vifo vya watoto Yemen

Umoja wa Mataifa umesema asilimia 51 ya vifo na majeraha ya watoto wadogo nchini Yemen mwaka uliopita, yamesababishwa na mashambulio ya anga yanayofanywa na ndege za muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala vamizi wa Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo maskini jirani yake.

Rasimu ya ripoti ya umoja huo ambayo inasubiri kuidhinishwa na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres imebainisha kuwa, watoto wadogo zaidi ya 680 wameuawa na kujeruhiwa katika hujuma hizo za anga mwaka jana pekee. 

Kadhalika ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, robo tatu ya mashambulizi dhidi ya shule na mahospitali yaliyoshuhudiwa mwaka jana nchini Yemen yalifanywa na muungano huo.  

Kauli ya UN imetolewa siku moja baada ya tovuti ya Al-Arabiyyul-Jadid kuripoti kuwa, watoto wadogo nchini Yemen ama wanauawa kwa vita au ugonjwa wa kipindupindu na endapo watanusurika na kubaki hai hukosa haki zao za kijamii na kisheria.

Watoto wa Yemen, wahanga wakuu wa hujuma za Aal-Saud

Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti hiyo, hadi sasa watoto 1,400 wameuawa na shule 2,000 zimebomolewa kutokana na mashambulio ya anga yaliyofanywa na Saudia dhidi ya nchi hiyo. 

Mashambulio ya anga ya usiku na mchana ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen tangu Machi mwaka 2015, hadi sasa yameshaua watu zaidi ya 12,000, na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makazi.

Madhumuni ya  vita hivyo vinavyoendelea kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu ni kuisambaratisha harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abd Rabbuh Mansur Hadi, kibaraka wa Aal Saud ambaye  alikuwa rais lakini akajiuzulu na kuitoroka nchi.