Vita vya Saudi Arabia dhidi ya watoto wa Yemen
Utangulizi wa ripoti iliyotayarishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kuhusu ukiukwaji wa haki za watoto katika migogoro ya vita umeutuhumu muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia kuwa umekiuka haki za watoto.
Shirika la habari na Ufaransa limefichua baadhi ya vipengee vya ripoti hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambayo itawasilishwa katika Baraza la Usalama la umoja huo hivi karibuni na kusema: Asilimia 51 ya vifo na majeraha ya watoto wadogo nchini Yemen mwaka uliopita yamesababishwa na mashambulio ya anga yanayofanywa na ndege za muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala vamizi wa Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo maskini na jirani. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, katika mwaka uliopita wa 2016 muungano vamizi wa Saudi Arabia umekiuka kwa kiango kikubwa haki za binadamu za watoto wadogo wa Yemen.
Hali ya sasa ya Yemen na ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto katika nchi hiyo kwa mara nyingine tena vimewafanya walimwengu waelekeze darubini na macho yo katika utendaji wa Umoja wa Mataifa katika kipindi hiki cha uongozi wa Antonio Guterres.yemen
Rekodi mbaya ya utendaji usiofaa wa taasisi hiyo ya kimataifa kuhusu maafa yanayowapata watu wa Yemen hususan ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto wadogo ingali hai katika fikra za walimwengu na Ban Ki-moon hakubakisha kumbukumbu mzuri ya Umoja wa Mataifa katika kipindi cha ukatibu wake mkuu kwenye jumuiya hiyo. Mauaji ya raia na ukiukaji mkubwa wa haki za watoto unofanywa na Saudi Arabia huko Yemen viliufanya Umoja wa Mataifa katika kipindi cha uongozi wa Ban Ki-moon kuuweka uwatala wa Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wakiukaji wa haki za watoto duniani. Hata hivyo mwezi Juni mwaka 2016 katibu huyo mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa alifadhilisha maslahi ya kisiasa badala ya uhai wa wanadamu na kufumbia macho ukiukaji huo mkubwa wa haki za binadamu za watoto kwa kuiondoa Saudi Arabia na washirika wake katika orodha hiyo nyesi baada ya serikali ya Riyadh kutishia kukata misaada yake ya kifedha kwa taasisi hiyo ya kimatifa. Hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa ni kielelezo halisi cha mtazamo wa kindumakuwili na kutumia haki za binadamu kama wenzo tu wa kukidhi malengo maalumu.
Baya zaidi ni kuwa, Saudia inayotambuliwa na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu kuwa ni nembo ya ukiukaji wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo, ilipewa uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa!
Kwa kutilia maanani hali mbaya na ya kusikitisha inayotawala Yemen na mauaji yanayoendelea kufanywa na wavamizi wa nchi hiyo hususan dhidi ya watoto na wananawake, walimwengu hawatarajii kingine kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonie Guterres ghairi ya kuiweka Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya nchi na taasisi zinazokiuka haki za watoto duniani.
Itakumbukwa kuwa siku chache zilizopita mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Yemen, Bismarck Swangin alisema waziwazi kwamba: "Vita ya Yemen ni vita dhidi ya watoto wanaosubiri kifo kutokana na utapiamlo na ugonjwa wa kipindupindu".