Saudia yawaweka katika orodha nyeusi shakhsia wanaoiunga mkono Qatar
Mshauri wa Kasri la Ufalme nchini Saudi Arabia ametangaza habari ya kukamilika maandalizi ya orodha eti nyeusi ya watu wanaoiunga mkono Qatar na siasa zake za kigeni kuhusu mgogoro wa uhusiano wa nchi hiyo na ya Saudia, Imarati, Bahrain na Misri.
Saud Al-Qahtani ameyasema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Twetter ambapo sambamba na kuashiria kuyaweka majina kadhaa ya raia wa nchi hiyo katika orodha hiyo nyeusi, amesema kuwa shakhsia hao watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Itakumbukwa kuwa Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao na Qatar tarehe tano mwezi Juni mwaka huu ambapo pia ziliiwekea mzingizo wa kila upande nchi hiyo ya Kiarabu.
Kufuata hatua hiyo, nchi hizo zilianza kuwatimua raia wa Qatar na kuwakamata, kuwafunga jela au kuwatoza faini watu ambao walionekana kuiunga mkono serikali ya Doha.
Hivi karibuni pia baadhi ya duru za habari vilifichua habari ya kutimuliwa baadhi ya mahujaji wa Qatar kutoka katika hoteli za maeneo yaliyo karibu na Msikiti wa Makkah na kutakiwa kwenda mbali na kwamba timuatimua hiyo ilikiuka haki za binadamu.
Nchi nne za Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zinaituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi, tuhuma ambazo zinapingwa na Doha.