Raia 35 wauawa katika mashambulio ya kijeshi ya Saudia nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33532-raia_35_wauawa_katika_mashambulio_ya_kijeshi_ya_saudia_nchini_yemen
Kwa akali watu 35 wameuawa nchini Yemen na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya anga ya ndege za kijeshi za utawala vamizi wa Saudi Arabia katika mji mkuu Sana'a.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2017 09:32 UTC
  • Raia 35 wauawa katika mashambulio ya kijeshi ya Saudia nchini Yemen

Kwa akali watu 35 wameuawa nchini Yemen na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya anga ya ndege za kijeshi za utawala vamizi wa Saudi Arabia katika mji mkuu Sana'a.

Kanali ya Televisheni ya al-Masirah imeripoti kwamba, maiti 30 zimepatikana katika kijiji cha Arhab baada ya ndege za kijeshi za Saudia kuyashambulia makazi hayo ya raia. Taarifa zaidi zinasema kuwa, kuna uwezekano wa idadi ya wahanga wa mashambulio hayo kuongezeka kutokana na hali ya idadi kubwa ya majeruhi kuwa mbaya.

Wakati huo huo, jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi vimejibu mashambulio na jinai hiyo ya Saudia kwa kushambulia kwa makombora maeneo kadhaa ya vikosi mamluki vya Saudia kusini mwa Yemen.

Mashambulio ya kijeshi ya Saudia huko Yemen yameua zaidi ya watu 12,000

Aidha wanajeshi watatu wa Saudia wameuawa na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen katika mikoa ya Jizan na Najran.

Mashambulio ya anga yanayofanywa mtawalia usiku na mchana na ndege za kivita za Saudi Arabia nchini Yemen yameshaua watu zaidi ya 12,000 hadi sasa, wakiwemo wanawake na watoto na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi tangu utawala huo wa Aal Saud ulipoanzisha vita dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka 2015 kwa madhumuni ya kuisambaratisha harakati ya wananchi ya Ansarullah  na kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi. Hayo yanajiri katika hali ambayo, asasi mbalimbali zimeendelea kutahadharisha kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika nchi hiyo.