Sayyid Nasrullah: Mapambano dhidi ya ugaidi yataendelea Lebanon
Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha nchini Lebanon amesema kuwa, mapambano katika milima ya mpakani mwa nchi hiyo na Syria yataendelea hadi yatakapoangamizwa kikamilifu magenge ya kigaidi.
Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo jana usiku wakati alipokuwa anatoa ufafanuzi kuhusu opereseheni ya pamoja ya jeshi la Syria na wanamapambano wa Hizbullah wa Lebanon katika milima ya mpakani mwa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa, operesheni hiyo inayofanyika kwa maelewano kamili na jeshi la Lebanon imefanikiwa kuwafurusha magaidi wa Daesh katika maeneo mengi ya Syria na Lebanon.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aidha amesema, tangu wiki iliyopita, wanamapbano wa Hizbullah kwa kushirikiana na jeshi la Syria walianzisha opereseheni ya kuwafurusha magaidi wa Daesh katika maeneo ya mpaka wa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa, licha ya kundi la Daesh kutumia raia kama ngao ya vita lakini jeshi la Lebanon na lile la Syria pamoja na vikosi vya muqawama vimepata ushindi mkubwa kwenye opereseheni hiyo.
Amesema ushindi mwingine mkubwa umekaribia nchini Lebanon kwani katika kipindi kifupi kijacho, magaidi wote watafurushwa katika mpaka mzima wa Lebanon na Syria na usalama kurejea katika ukanda wote wa mpakani.
Aidha amewaambia viongozi wa genge la kigaidi la Daesh kuwa ushindi wa jeshi la Syria, la Lebanon na vikosi vya muqawama katika operesheni ya kuikomboa milima ya mpakani mwa nchi hizo mbili ni jambo lisilozuilika tena, hivyo wasijidanganye kudhani kuwa wataweza kuzuia ushindi huo.