Saudia yawatishia Walebanon kwa hatua yao ya kuiunga mkono Hizbullah
Saudi Arabia imetoa radiamali ikijibu nafasi ya hivi karibuni ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah ya kutoa pigo kwa makundi ya kigaidi mashariki mwa nchi hiyo kwa kuwatishia wananchi wa Lebanon kutokana na hatua yao ya kuiunga mkono harakati hiyo ya Kiislamu.
Thamer al Sabhan Waziri Mshauri wa Saudia katika Masuala ya Nchi za Eneo la Ghuba ya Uajemi aliandika jana katika ukurasa wake wa twitter kuwa Walebanoni wanapasa imma waichague Hizbullah au wawe dhidi yake. Waziri huyo wa Saudia amedai kuwa harakati ya Hizbullah inapasa kulipa gharama za hatua zake hizo.
Gazeti la al Akhbar la Lebanon limeashiria ujumbe huo wa vitisho wa al Sabhan sambamba na kuanza maneva ya utawala wa Kizayuni katika mpaka wa Lebanon na kuandika kuwa, Saudi Arabia imeamua kutekeleza siasa za vitisho vya waziwazi baada ya harakati ya Hizbullah pamoja na jeshi la Lebanon kutoa pigo kwa kundi la kigaidi la Daesh.
Waziri Mshauri wa Saudi Arabia katika Masuala ya Nchi za Eneo la Ghuba ya Uajemi wiki mbili zilizopita alifanya safari huko Beirut mji mkuu wa Lebanon na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi na shaksia wa kisiasa akiwemo Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri, Sami al Gemayel Kiongozi wa Chama cha al Kataib na Samir Jaajah Kiongozi wa chama cha Lebanese Forces.