Aslimia 85 ya ardhi ya Syria imekombolewa toka mikononi mwa magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34279-aslimia_85_ya_ardhi_ya_syria_imekombolewa_toka_mikononi_mwa_magaidi
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa asilimia 85 ya ardhi yake iliyokuwa ikidhibitiwa na magenge ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2017 22:02 UTC
  • Aslimia 85 ya ardhi ya Syria imekombolewa toka mikononi mwa magaidi

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa asilimia 85 ya ardhi yake iliyokuwa ikidhibitiwa na magenge ya kigaidi.

Luteni Jenerali Aleksandr Lapin, Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Russia nchini Syria jana Jumanne alisema kuwa, kwa sasa jeshi la Syria likishirikiana na vikosi waitifaki lina kibarua cha kukomboa asilimia 15 tu ya ardhi yake, ambayo ni sawa na kilomita mraba 27,000.

Ameongeza kuwa, wanachama zaidi ya 450 wa makundi ya kigaidi nchini Syria waliuawa katika operesheni ya hivi karibuni ya kuvunja mzingiro wa mji wa Deir ez Zor.

Jeshi la Syria Jumanne ya wiki iliyopita lilitangaza kuwa limefanikiwa kuvunja mzingiro katika mji wa Deir ez Zor mashariki mwa nchi hiyo ambao ulidhibitiwa na wanamgambo wa Daesh karibu miaka mitatu iliyopita na kuingia umbali wa kilomita tatu mjini humo.

Vikosi vya Syria katika operesheni ya nchi kavu

Wadadisi wa mambo wanasema kuvunjwa mzingiro wa mji huo ni mwanzo wa mwisho wa harakati za magenge ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Syria ilianza kukabiliwa na mgogoro mwaka 2011 kufuatia hujuma kubwa za makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao ili kuipindua serikali halali ya Rais Bashar Assad wa Syria.